Home Mchanganyiko TAASISI ZA UMMA NCHINI ZATAKIWA KUWAPATIA HUDUMA YA USAFIRI WATUMISHI WA...

TAASISI ZA UMMA NCHINI ZATAKIWA KUWAPATIA HUDUMA YA USAFIRI WATUMISHI WA UMMA WENYE ULEMAVU

0

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary M. Mwanjelwa (Mb) akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Amina S. Mollel  Bungeni leo jijini Dodoma, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora lililohusu  mpango  wa Serikali wa kuwapatia huduma ya usafiri Watumishi wa Umma wenye Ulemavu.

*******************************

Happiness Shayo-Dodoma

Tarehe 14 Novemba, 2019

Serikali imezitaka Taasisi za Umma nchini kuhakikisha zinatatua changamoto ya
huduma ya usafiri kwa Watumishi wa Umma wenye Ulemavu ili waweze
kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) kwa niaba ya Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Kapt (Mst) Mhe. George Mkuchika wakati akijibu swali la Mhe. Amina S. Mollel
(Mb) (Viti Maalum) aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuwapatia
huduma ya usafiri Watumishi wa Umma wenye Ulemavu.

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema kuwa, ili kufanikisha azma hiyo ya Serikali,
Taasisi za Umma zinatakiwa kutekeleza miongozo inayotolewa ikiwa ni pamoja
na Mwongozo wa Huduma kwa Watumishi wa Umma Wenye Ulemavu wa
mwaka 2008 unaoelekeza Waajiri kuwapatia huduma ya usafiri au kulipia
gharama za mafuta ya kwenda na kurudi kazini kwa Watumishi wa Umma wenye
Ulemavu ambao wana vyombo binafsi vya usafiri, lengo likiwa ni kuwawezesha
kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Mhe. Dkt. Mwanjelwa ameongeza kuwa, Waajiri ambao hawatekelezi Mwongozo
huo, wanakiuka maelekezo ya Serikali kwa kuwanyima stahiki watumishi wenye
ulemavu, hivyo wakibainika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za
kiutumishi zilizopo.

Serikali kupitia Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini imejipanga kufanya Ufuatiliaji wautekelezaji wa Mwongozo huo ili uweze kufanya kazi kama ilivyokusudiwa.

Aidha, Dkt. Mwanjelwa amewakumbusha Waajiri kutoa kipaumbele cha mikopo
ya vyombo vya usafiri kwa Watumishi wa Umma Wenye Ulemavu wanaokidhi
vigezo vya kukopesheka ikiwa ni utekelezaji wa Waraka wa Watumishi wa
Serikali Na.3 wenye Kumb.Na. C/AC.7/228/01/16 wa Juni 30, 2011 unaotoa
Utaratibu wa Kukopesha Fedha Taslimu Watumishi wa Serikali kwa ajili ya
kununulia Magari au Pikipiki pamoja na Matengenezo ya Magari na Pikipiki hizo.