Home Mchanganyiko CHAMA CHA WALIMU WAUNGA MKONO MAELEKEZO YA RAIS MAGUFULI MKOANI SONGWE

CHAMA CHA WALIMU WAUNGA MKONO MAELEKEZO YA RAIS MAGUFULI MKOANI SONGWE

0

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela akimshukuru Katibu wa CWT Mkoa wa Songwe Bi Emilia Mwakyoma kwa niaba ya CWT Taifa kwa mchango wa mifuko 400 ya saruji itakayosaidia katika kuboresha miundombinu ya madarasa Mkoa wa Songwe. Katikati ni Afisa Elimu Mkoa wa Songwe Juma Kaponda.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Mbozi John Palingo (aliyevaa kofia) kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Songwe mchango wa Chama cha Waalimu Nchini (CWT) mifuko 400 ya saruji kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu Mkoani Songwe.

……………………

Chama cha Waalimu Tanzania (CWT) kimeunga Mkono maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ya ukamilishaji wa maboma ya Vyumba vya madarasa, kwa kuchangia Mifuko 400 ya saruji Mkoa wa Songwe.

Katika ziara yake Mkoa wa Songwe Rais Magufuli alipokea taarifa ya bakaa ya shilingi billioni Mbili ambapo alielekeza fedha hizo zitumike kukamilisha mabomba ya shule ambayo yamejengwa kwa nguvu za wananchi hususani katika Wilaya ya Mbozi.

Akikabidhi mchango huo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CWT, Katibu wa CWT Mkoa wa Songwe Bi Emilia Mwakyoma amesema Chama cha Waalimu kinapongeza Serikali kwa kuhimiza uboreshaji wa miundombinu ya Elimu.

“Tunapongeza sana Juhudi za Serikali ya awamu ya tano na sisi kama wadau wa elimu tumechangia na tutaendelea kuchangia kwakuwa tunatambua kuwa serikali inatengeneza miundombinu mizuri ya wanafunzi kujifunzia pia waalimu watakuwa na mazingira mazuri ya kufanyia kazi.”, amesema Mwakyoma.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela ameipongeza CWT kwakuwa licha ya kutetea haki za waalimu wamekuwa mstari wa mbele katika kuthamini na kuchangia miundombinu ya elimu hasa kwa Mkoa wa Songwe.

Brig. Jen. Mwangela amesema mchango huo unapelekwa maeneo yenye uhitaji Zaidi huku akieleza kuwa Wilaya ya Mbozi mpaka sasa ina maboma 1510 hivyo wadau wengine wajitokeze kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu Mkoani Songwe.

Naye Afisa Elimu Mkoa wa Songwe Juma Kaponda amesema kwa Mkoa wa Songwe jumla ya maboma 1601 yanaendelea kujengwa huku halmashauri ya Mbozi ikiongoza kwa kuwa na maboma mengi yaani 1510.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Msanyila Wilayani Mbozi Gwakisa Mwalusaku amesema shule hiyo imejenga vyumba 16 ambapo mifuko kumi ya saruji waliyopokea kutoka CWT itaharakisha ukamilishaji wa vyumba hivyo.