Home Mchanganyiko MNYETI AWAKABIDHI PIKIPIKI WATENDAJI KATA BABATI MJINI

MNYETI AWAKABIDHI PIKIPIKI WATENDAJI KATA BABATI MJINI

0
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amewakabidhi pikipiki watendaji sita kati ya nane wa Kata za Mjini Babati, waliokuwa wanafanya kazi zao kwa changamoto ya ukosefu wa usafiri, ili kuwafikia na kuwatumikia wananchi wengi zaidi. 
Pikipiki hizo sita zenye thamani ya sh14.3 milioni zimenunuliwa na halmashauri ya mji wa Babati, kupitia fedha za kujenga uwezo zinazotokana na kuendeleza miji (ULGSP).
Mnyeti akiwakabidhi maofisa watendaji hao wa kata sita za mjini Babati, alisema vitendea kazi hivyo viwe nyenzo za kuwafikia wananchi zaidi tofauti na awali. 
Alisema watendaji kata hao waliopo pembezoni mwa mji wa Babati wanapaswa kutokaa ofisini na kuwafikia wananchi kuwatumikia ili kuondokana na kisingizio cha ukosefu wa usafiri. 
“Tunataka tuone kero za wananchi zinatatuliwa, kama mimi nafika hadi vijijini, ninyi watendaji wa kata au vijiji mnapaswa kufika hadi kwenye ngazi ya kaya na kutatua changamoto zao,” alisema Mnyeti. 
Hata hivyo, alimuagiza mkurugenzi wa mji wa Babati, Fortunatus Fwema kuhakikisha maofisa watendaji wa kata za Babati na Bagara, nao wananunuliwa pikipiki kama wenzao.
Fwema alisema wapo kwenye mchakato wa kuhakikisha wanawanunulia pikipiki watendaji wa kata za Babati na Bagara. 
“Baada ya kuwanunulia pikipiki watendaji wa kata zilizo pembezoni tunaahidi kutekeleza agizo lako la kuwanunulia watendaji wawili wa Babati na Bagara ili kukamilisha kata zote nane,” alisema Fwema. 
Ofisa utumishi wa halmashauri ya mji wa Babati, Sadiki Mrisho alisema pikipiki hizo zinapaswa kutumiwa na maofisa watendaji wa kata sita kwa matumizi ya serikali pekee. 
Mrisho alisema pikipiki hizo zimetolewa kwa mkopo kwa watendaji hao utakaosaidia utunzaji na ununuzi wa pikipiki nyingine. 
Ofisa mtendaji wa kata ya Sigino, Evelin Panga alisema pikipiki hizo zitawasaidia kufika kiurahisi katika shughuli zao vijijini. 
Panga aliishukuru serikali kwa kuwapatia nyenzo hizo za usafiri kwani awali walikuwa wanatembea kwa miguu kutoka sehemu moja hadi nyingine.