Home Mchanganyiko GIDABUDAY AKABIDHI RASMI OFISI RT

GIDABUDAY AKABIDHI RASMI OFISI RT

0

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday (wa pili kushoto), akimkabidhi baadhi ya nyaraka Kaimu Katibu Mkuu, Ombeni Zavala (kushoto), wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, juzi. Wanaoshuhudia kutoka kulia ni Aziza Pembe, John Steven (wahudumu), na Rahel Swai (Katibu Muhtasi).

******************************************

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday, amekabidhi rasmi ofisi ya shirikisho hilo baada ya kujiuzulu hivi karibuni.

Gidabuday, alijiuzulu wadhifa huo kwa maslahi mapana ya RT Novemba Mosi, katika kikao cha Kamati Tendaji kilichofanyika jijini Dar es Salaam, ambacho kiliridhia uamuzi huo.

Makabidhiano hayo yalifanyika juzi katika ofisi za Shirikisho hilo, Temeke jijini Dar es Salaam, mbele ya Kaimu Katibu Mkuu, Ombeni Zavala, Makamu wa Kwanza wa Rais Utawala na Fedha, William Kallaghe na wafanyakazi wa shirikisho hilo.

Makabidhiano yalihusisha nyaraka mbalimbali, vifaa na madeni huku baadhi ya nyaraka chache zilizosalia Katibu huyo aliyejiuzulu akiahidi kumalizia kuzikabidhi ndani ya wiki moja.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Gidabuday alisema anashukuru anaondoka RT salama na kuahidi kuendelea kuwa mwanafamilia mwema wa Riadha.

“Nashukuru Wajumbe wa Kamati Tendaji kwa kunikubalia kujiuzulu kwangu kwa moyo mmoja, hivi sasa nitakuwa na muda wa kutosha na niko tayari kutoa mchango wangu pale nitakapohitajika,” alisema Gidabuday na kuongeza hivi sasa atakuwa anapatikana mkoani Arusha na Manyara akijishughulisha na kuandaa maandiko mbalimbali ya miradi ya michezo na kukuza vipaji hususan mkoani Manyara.

Naye Kaimu Katibu Mkuu, Zavala, aliwaondoa hofu wanafamilia ya Riadha hususan wachezaji kuwa wasisite kumuona pale watakapokuwa wakihitaji msaada.

Zavala, aliwaomba wajumbe wa Kamati Tendaji, kumpa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu ya shirikisho hilo.

RT inatarajiwa kufanya mkutano wake mkuu Desemba mwaka huu, ambako katika moja ya ajenda itakuwa mabadiliko ya Katiba, ikiwamo kuwa Mtendaji Mkuu (CEO), badala ya katibu wa kuchaguliwa.