Home Mchanganyiko TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA 18 WA MAWAZIRI WA MAMBO ...

TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA 18 WA MAWAZIRI WA MAMBO YA NJE WA NCHI 29 ZA AFRIKA NA NCHI 5 ZA NORDIC, KUANZIA TAREHE 7- 8 NOVEMBA 2019

0

Balozi wa Swedeni nchini Tanzania Bi.Anders Sjoberg akiongea na Wanahabari katika mkutano uliofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam leo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Faraja K. Mnyepe akiongea na Wanahabari katika mkutano uliofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam leo.

*****************************

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika 29 na nchi 5 za Nordic unaotarajiwa kufanyika tarehe 08 Novemba 2019, kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Wanahabari Jijini Dar es Salaam leo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Faraja K. Mnyepe amesema kuwa Mkutano huu utafunguliwa rasmi naMheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huu mkubwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000.

Aidha Dkt. Mnyepe amesema kuwa Mkutano huo utajumuisha jumla ya Mawaziri 34 wa Mambo ya Nje wa nchi za Afrika na Nordic pamoja na washiriki wengine ambao idadi yao inatarajiwa kufikia 250.

“Mawaziri watakaokuja kutoka nchi za Nordic ni wa nchi za Sweden, Norway, Denmark, Finland na Iceland. Kutoka nchi za Afrika watakuja Mawaziri wa Algeria, Angola, Benin, Botswana, Burkina Faso, Burundi, Comoros, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC), Misri, Ethiopia, Ghana, Kenya, Lesotho, Mali, Malawi, Morocco, Msumbiji, Namibia, Nigeria, Niger, Rwanda, Senegal, Somalia, Afrika Kusini, Tunisia, Uganda, Zambia, Zimbabwe na sisi wenyeji Tanzania”. Amesema Dkt.Mnyepe.

Amesema mkutano huo utajumuisha Mawaziri, Mabalozi wa nchi shiriki za Afrika katika nchi za Nordic, Mabalozi wa nchi za Nordic hapa nchini pamoja na watendaji wa Serikali. Kauli mbiu ya mkutano huu kwa mwaka huu ni: Ushirikiano kwa Maendeleo Endelevu (Partnering for Sustainable
Development).

Hivyo Dkt.Mnyepe amesema kuwa Ushirikiano kati ya Tanzania na nchi za Nordic ni wa kihistoria na wa kipekee na vilevile Ushirikiano huu ulianza hata kabla ya uhuru wa Tanganyika ambapo Wamisionari kutoka nchi hizo walikuja kufanya kazi hapa nchini kwenye sekta za afya na elimu.

Katika sekta ya elimu, nchi hizo zilianzisha Kituo cha Kilimo cha Uyole na Kituo cha Elimu cha Kibaha kupitia Mradi wa Nordic-Tanganyika Project. Ushirikiano wa karibu kati ya Tanzania na nchi za Nordic ulichangiwa kwa kiwango kikubwa na falsafa zilizokuwa zinafanana kuhusu maendeleo ya watu, ukombozi wa Afrika, urafiki miongoni mwa viongozi wetu na nafasi ya kimkakati ya Tanzania katika Bara la Afrika.

“Katika nchi za Afrika, Tanzania inapokea misaada mingi kutoka nchi za Nordic kuliko nchi nyingine yoyote. Kwa mfano kwa miaka mitano ya kuanzia mwaka 2013 hadi 2018, Tanzania imepokea takribani Shilingi za Kitanzania bilioni 900 kutoka nchi za Nordic. Nchi hizo zimekuwa zikisaidia sekta mbalimbali hapa nchini ikiwemo: elimu; afya; miundombinu; nishati; TEHAMA; utafiti; ukusanyaji wa kodi; bajeti; misitu; usawa wa jinsia; utunzaji wa mazingira; na ukuzaji wa sekta ya biashara”. Amesema Dkt.Mnyepe.

Amesema kuwa wazo la kuanzisha mkutano huu lilianza mwaka 2000 ambapo mkutano wa kwanza ulifanyika nchini Sweden mwaka 2001. Baada ya hapo mikutano kama hii inafanyika kwa kupokezana kutoka Bara la Afrika na upande wa Nordic. Mwaka 2017, mkutano ulifanyika Abuja, ambapo mambo mbalimbali ya kiushirikiano yamekuwa yakijadiliwa kirafiki na kuelewana zaidi na hatimaye mikakati ya pamoja inawekwa kwa ajili ya utekelezaji. Masuala hayo ni pamoja yale yanayohusu biashara, uwekezaji, mikakati ya kisekta na hasa inayochochea ukuaji wa haraka wa uchumi na utoaji wa ajira.

 

Ameongeza kuwa mikutano hii inajadili masuala ya amani na usalama katika kanda na duniani pamoja na masuala mengine ya kidunia yenye maslahi kwa nchi za Afrika na Nordic ikiwemo masuala yanayohusu mabadiliko ya tabianchi.