Home Mchanganyiko RC SINGIDA AFUNGUA MKUTANO MKUU WA TATU WA CHAMA KIKUU CHA USHIRIKA...

RC SINGIDA AFUNGUA MKUTANO MKUU WA TATU WA CHAMA KIKUU CHA USHIRIKA (SIFACU LTD)

0

 Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt.Rehema Nchimbi, akihutubia wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Tatu wa Chama Kikuu cha Ushirika (SIFACU Ltd) mkoani hapa juzi. Kutoka kushoto ni Katibu Tawala Msaidizi Uzalishaji Mkoa wa Singida, Beatus Choaji,  Mkuu wa Wilaya ya Singida,  Mhandisi Paskasi Muragili, Mwenyekiti wa  chama kikuu cha ushirika mkoa wa Singida,  Khamis  Mwanjowa na  mrajisi msaidizi wa  vyama vya ushirika mkoa wa Singida,  Thomas Nyamba.
 Mrajisi msaidizi wa  vyama vya ushirika mkoa wa Singida,  Thomas Nyamba, akizungumza katika mkutano huo.
 Mwenyekiti wa  chama kikuu cha ushirika mkoa wa Singida,  Khamis  Mwanjowa, akizungumza.
 RC Nchimbi na wajumbe wa mkutano huo wakiserebuka.
 RC Nchimbi na wajumbe wa mkutano huo wakiserebuka.
 Mkutano ukiendelea.
 Mkutano ukiendelea. 
 RC Nchimbi akikagua bidhaa za wajasiriamali.
 Wajumbe wakiwa kwenye mkutano huo.
 Wajumbe wakiwa kwenye mkutano huo.
Picha ya pamoja. 
 
 
Na Waandishi Wetu, Singida
 
 
MKUU wa Mkoa wa Singida, Dkt.Rehema Nchimbi ametoa miezi miwili kwa Mrajisi wa Vyama vya Ushirika mkoani hapa kuhakikisha anafanya ukaguzi kwa vyama vyote ambavyo bado havijakaguliwa, na kinyume chake hataruhusu mchakato wowote wa mikopo kufanyika.
 
Dk.Nchimbi aliyasema hayo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa tatu wa Chama Kikuu cha Ushirika (SIFACU Ltd) mkoani hapa juzi.
 
“Ukaguzi kwenye vyama hivi ni lazima na sio hiari, nakuagiza mrajisi ndani ya miezi miwili vyama vyote  vilivyobaki viwe vimekaguliwa na  chama kisichokaguliwa kisipewe mkopo wowote,” alisema Nchimbi
 
Alisema kwa mkoa wa Singida inasikitisha kuona takwimu zinaonyesha kati ya jumla ya vyama 320 vilivyopo ni vyama 70 pekee ndivyo vilivyokaguliwa jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali chanya  wa uhai wa ushirika na wanaushirika wenyewe.
 
Alisisitiza kuwa, ushirika pamoja na mambo mengine ni lazima utembee na ajenda ya mshikamano, nguvu, heshima na uhai endelevu sanjari na kuweka kando masuala yote yanayoweza kuufifisha ikiwemo ubinafsi na migogoro isiyokoma.
 
“Utakuta kila siku  vitu vinavyoleta utapiamlo kwenye vyama hivi vya ushirika ni ubinafsi…watu wamesahau kabisa kuwa ushirika ni utumishi ndio maana rushwa imetamalaki na matokeo yake ni kufifisha matarajio yake chanya,” alisema
Nchimbi
 
Alisema anatamani moja ya ajenda kubwa ya wanaushirika wote iwe ni kutafuta suluhisho la lishe bora kwa watoto waliopo mashuleni ili hatimaye kuwawezesha kujenga utulivu wa akili kuweza kumsikiliza vizuri mwalimu na kumudu masomo yao.
 
Dkt. Nchimbi aliwakumbusha wana ushirika wote nchini, hususan wale wa mkoa wa Singida kutambua kwamba wao ni nguzo na mkono wa serikali katika kushauri, kuongoza, kuelekeza na kuifikisha jamii na taifa kwenye uchumi wa viwanda kama ishara na tunda la serikali iliyopo madarakani kwa sasa.
 
Kwa upande wake, Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoani hapa, Thomas Nyamba, alisema hali ya vyama vya ushirika ndani ya mkoa wa Singida inaendelea kuimarika ikilinganishwa na huko nyuma, huku idadi ya vyama hivyo ikifikia 320
 
“Tuna jumla ya vyama vya ushirika mia tatu na ishirini, kati ya hivyo sitini na tisa ni vile vya mazao hususan pamba, huku upande wa saccos hali sio ya kuridhisha kutokana na vingi kati yake kukabiliwa na madeni,” alisema Nyamba
 
Makamu Mwenyekiti wa SIFACU, Yahaya Ramadhan Khamis alibainisha pamoja na mambo mengine lengo la mkutano huo mkuu ni kutathmini shughuli zote zilizofanywa kwa mwaka uliopita na kupanga mipango ya mwaka unaoanza
 
“Mwaka uliopita tumefaulu kuunganisha vyama na wanachama wakekutoka idadi ya vyama thelathini na sita hadi sitini na sita, tumeweza pia kutafuta masoko ya uhakika, kuwaunganisha wakulima kuweza kupata mikopo kwenye taasisi mbalimbali za fedha,” alisema Khamis