Home Mchanganyiko KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA e-GA

KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA e-GA

0

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge, Tawala na Serikali za Mitaa Mhe.Mwanne Ismail Nchemba akifafanua jambo wakati wa kikao na Menejimenti ya Wakala Oktoba 30, 2019 katika Makao Makuu ya e-GA DODOMA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Kapt. (Mst) George H. Mkuchika (Mb) akielezea manufaa ya TEHAMA kwa Serikali na wananchi wakati wa Kikao na Menejimenti ya Wakala leo Oktoba 30, 2019 katika Makao Makuu ya e-GA DODOMA

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao Dkt. Jabiri Kuwe Bakari akiwaelezea wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge, Tawala na Serikali za Mitaa jinsi mifumo ya TEHAMA inavyorahisisha Utendaji Kazi Serikalini na Utoaji Huduma kwa Umma

Wanakamati wa Kamati ya kudumu ya Bunge, Tawala na Serikali za Mitaa wakiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti pamoja na watumishi wa Wakala ya Serikali Mtandao DODOMA mara baada ya kikao leo Oktoba 30, 2019

………………..

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge, Tawala na Serikali za Mitaa Mhe. Mwanne Ismail Nchemba amesema Serikali inaitegemea Wakala ya Serikali Mtandao (e-GA) kubuni zaidi njia za kurahishisha utendaji wa shughuli za Serikali kwa kutumia TEHAMA. 

Amesema hayo wakati wa kikao cha pamoja kati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge, Tawala na Serikali za Mitaa na Mejimenti ya Wakala kilichofanyika tarehe 30 Oktoba, 2019 Makao Makuu ya ofisi za Wakala zilizopo mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma.

Sisi kama Kamati tunawapongeza na tunatambua jitihada mnazofanya katika kuhakikisha Serikali inakuwa ya kimtandao ili kupunguza gharama za uendeshaji kwa Serikali na kutoa huduma kwa umma mahali popote  na kwa gharama nafuu” Amesema Mhe. Mwanne Ismail Nchemba.

Aidha, Kamati hiyo kwa jumla imetoa pongezi kwa Wakala kwa kazi inazofanya hasa za kuhakikisha Serikali inatumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano yaani TEHAMA katika ukusanyaji mapato na kupunguza gharama za utoaji huduma kwa umma.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt. (Mst) George H. Mkuchika (Mb) amewataka watumishi wa Wakala kuongeza bidii zaidi katika kazi kwa kuwa dunia ya sasa inategemea sana TEHAMA katika utendaji kazi.

“Tambueni kuwa Serikali Mtandao imesaidia katika ukusanyaji wa mapato Serikalini na kadiri mapato yanavyoongezeka, ndivyo Serikali inavyoweza kuwahudumia wananchi kwa urahisi na kwa wakati” ameongeza Mhe. Mkuchika.

Pia amesisitiza kuwa watumishi wa Wakala wanatakiwa kutambua kuwa nafasi yao ni kubwa katika kufikia malengo ya Wakala na azma ya Serikali ya kutumia TEHAMA katika shughuli zake mbalimbali.

Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao, Dkt. Jabiri Kuwe Bakari ameiambia Kamati hiyo kuwa kwa kutumia wataalamu wa ndani, Wakala imetengeneza mifumo mbalimbali kama vile Mfumo wa Ukusanyaji Mapato Kielektroni (GePG), Mfumo wa Ofisi Mtandao (e-Office), Mfumo wa Baruapepe Serikalini (GMS), Mfumo Shirikishi wa Kusimamia Shughuli na Rasilimali za Taasisi (ERMS), Mfumo wa Vibali vya Kusafiri Nje ya Nchi (e-Vibali) pamoja na mifumo mingine ili kurahisisha utendaji kazi Serikalini na utoaji huduma kwa umma.

Vilevile, Mkurugenzi wa Uratibu wa Miundombinu ya TEHAMA Bw. Benjamin Dotto amesema kuwa Wakala hiyo imeunganisha kwa data na sauti Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala na Mamlaka za Serikali za Mtaa katika Mtandao mmoja wa Mawasiliano wa Serikali ambao ni salama na mtandao huo umeunganishwa katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Amesisitiza mbele ya Kamati hiyo kuwa, Wakala ina wataalamu wa ndani wanaofuatilia mtandao huo  kwa karibu na inapobainika tatizo au changamoto yoyote wataalam hao hushughulikia kwa haraka ili kutoathiri utendaji kazi.