Home Mchanganyiko WANAWAKE WAPEWA MBINU ZA KUSHINDA UCHAGUZI

WANAWAKE WAPEWA MBINU ZA KUSHINDA UCHAGUZI

0
Na: Mwandishi Wetu 
WANAWAKE wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma waliotia nia ya kugombea uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika nchini Tanzania, Novemba 24, 2019 toka vyama vya siasa wamepewa mbinu za kushinda uchaguzi huo kwa wingi na kishindo.
Wanawake 64 wamepewa mafunzo na Shirika lisilo la Kiserikali la Tanzania Gender Networking  Programme (TGNP) la Dar  es Salaam,  kwa lengo la kuwajengea uwezo wanawake waliotia nia katika kinyang’anyiro  cha Uchaguzi
wa serikali za mitaa wakiwa na moto wao wa “Wanawake wakati  wa kuongoza ni sasa.
Kwa mujibu wa Waziri wa  Nchi Ofisi ya Rais  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,  Selemani Jafo (MB), maandalizi ya awali ya uchaguzi wa serikali za mitaa yamekamilika kwa kuzingatia kanuni za Uchaguzi wa serikali za Mitaa wa Mwaka 2019 Ibara ya 4 (1-3).
Mwezeshaji wa Mafunzo hayo toka TGNP, ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere Dar es Salaam, Bw. Henry Kigodi amesema: TGNP imejikita kusaidia wanawake ambao wametia nia katika kugombea nafasi mbalimbali ili kukidhi hitaji la kupata viongozi wanawake wengi ambao kwa kipindi kirefu hushindwa kufanikiwa kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukosa mbinu za kampeni na kukabiliana na mfumo dume.
Bw. Kigodi alisema wanawake wakipata uongozi huwa makini katika maamuzi, kutekeleza na kusimamia shughuli za kimaendeleo kwakuwa wanawake huwa wanakabiliwa na changamoto nyingi  za kimaendeleo katika vitongoji, vijijiji na
mitaa yao. “Wanawake ndio wanaohangaika na changamoto za ukosefu wa maji,  huduma za afya na Malezi lakini wao ndio hushiriki kwa kiwango kikubwa katika shughuli za uzalishaji mali kama kilimo na hawafaidi matunda yake,” alisema Kigodi.
Mwezeshaji wa Mafunzo  Bw. Henry Kigodi akifafanua jambo katika mafunzo
Naye, mwezeshaji Mwenza Gratiana Rwakibarila, alisema ni vema wanawake wakatambua kuwa wana uwezo mkubwa katika kuongoza jamii na hivyo wanawajibu mkubwa katika kuhakikisha wanapata mbinu za kushinda nafasi walizoziomba kwa kupewa mafunzo ya  kujijengea uelewa wa pamoja juu ya ushiriki katika uchaguzi.
Mwezeshaji Gratiana Rwakibarila akiwa anaeleza namna ya kuboresha mbinu za kampeni 
Vilevile alisema, wanawake lazima wajengewe uelewa wa dhana za jinsia ili kuwawezesha watia nia kuzihusisha na maswala ya uchaguzi, kujadili umuhimu katika ushiriki wa wanawake katika kampeni na uchaguzi. Aidha, Gratiana alisema mafunzo hayo yatawaboreshea mbinuzao za mikakati na mbinu za  kampeni wakati wa uchaguzi.
Jumla ya vyama vitano vya siasa vinashiriki mafunzo hayo, vyama hivyo ni ADA- TADEA, CCM, CHADEMA, CUF na TLP. Washiriki wamesisitizwa kuwa wakishinda wayaangalie maendeleo kwa mtazamo wa kijinsia na kupambana na sera potofu za kijinsia.

Washiriki wa mafunzo wakiwa katika vikundi vya mijadala