Home Mchanganyiko TANZANIA KUADHIMISHA SIKU YA UMOJA WA MATAIFA (UN) KESHO JIJINI DODOMA

TANZANIA KUADHIMISHA SIKU YA UMOJA WA MATAIFA (UN) KESHO JIJINI DODOMA

0

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Faraji Mnyepe,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu siku ya maadhimisha ya Umoja wa Mataifa (UN) yatakayofanyika kesho jijini Dodoma

Kaimu Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa hapa nchini, Balozi Michael Dunford,akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dodoma wakati akizungumzia siku ya  maadhimisha ya Umoja wa Mataifa (UN) yatakayofanyika kesho jijini Dodoma

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Faraji Mnyepe akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa umoja wa mataifa (UN)

………………..

Na.Alex Sonna,Dodoma

TANZANIA itaungana na nchi zingine ulimwenguni kesho kuadhimisha siku ya Umoja wa Mataifa(UN) katika viwanja vya Nyerere jijini Dodoma.

Akizungumza leo na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk.Faraji Mnyepe, amesema Waziri Prof.Palamagamba kabudi ndio atakayekuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo yenye kauli mbiu kuwa ‘Wanawake na wasichana kuwa kipaumbele katika kufikia malengo ya Dunia’.

Amesema yatahusisha upandishaji bendera ya UN pamoja na paredi ya Jeshi la Ulinzi Tanzania(JWTZ), na kwamba kauli mbiu hiyo inaweka mkazo katika kuleta maendeleo yanayozingatia usawa wa kijinsia kwa kutomuacha mtu nyuma.

“Serikali kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa tumekuwa tukishirikiana katika kuweka mazingira wezeshi ya wote kujiendeleza kupitia programu mbalimbali za UN, Wanawake sio tu chanzo cha maisha yetu wote bali ni sehemu kubwa ya nguvu kazi ya Taifa hususan vijijini,”amesema

Katibu huyo amesema kutokana na hilo wanapaswa kupewa fursa, vipaumbe katika masuala yote ya maendeleo ili kufikia Malengo endelevu ya Dunia(SDGs) yanayolenga kutomuacha mtu yeyote nyuma.

Naye, Mwakilishi wa UN nchini, Michael Dunford, amesema kesho ni maadhimisho ya miaka 74 ya Umoja huo ambapo nchi 50 awali ndio zilizoanzisha umoja huo lakini kwasasa zipo nchi 193.

“Kesho tunasherehekea hapa Dodoma kwa kazi kubwa iliyofanywa na UN lakini pia ushirikiano wetu na Tanzania, na ni mara ya kwanza kusherehekea hapa tangu serikali ihamishie Makao Makuu yake Dodoma,”amesema

Amesema ili kufikia Malengo endelevu ya Dunia(SDGs) ifikapo mwaka 2030 ni muhimu kuzingatia usawa wa kijinsia ili itasaidia kufanikiwa katika malengo mengine 17.

Amebainisha kuwa kuna umuhimu wa kuwekeza kwa wanawake na wasichana kwa kuwapa fursa ili kufanikiwa kiuchumi na kijamii.

“Nitoe wito kwa watanzania kuhudhuria kwa wingi kwenye maadhimisho haya ili kuthibitisha ushirikiano na mashikamano tuliyonayo kwa UN katika kujiletea maendeleo,”amesema.