Na Nuru Ikupa, DSM
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, amesema Tanzania inaungana na mataifa mbalimbali duniani katika kuhakikisha kuwa dunia inakuwa ni mahala salama pa kuishi na ili kufiki athma hiyo Tanzania inashirikiana na nchi nyingine duniani kuweka juhudi za pamoja katika udhibiti wa uharibifu wa mazingira na matumizi ya kemikali hatarishi.
Naibu Waziri Nyongo alisema, Tanzania imesaini Mkataba ujulikanao kama Minemata wenye lengo la kudhibiti matumizi ya kemikali ya zebaki inayotumika kukamata dhahabu kutokana na athari ya kemikali hiyo kwa jamii na mazingira kwa ujumla.
Alisema mkataba huo unawataka nchi wanachama kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030 matumizi ya zebaki katika kukamata dhahabu yanafikia mwisho na njia mbadala inapatikana.
Nyongo aliyasema hayo jana tarehe 18 Oktoba, 2019 alipokuwa katika mahojiano ya moja kwa moja katika studio za TBC Taifa jijini Dares Salaam alipoalikwa ili kuzungumzia dhana ya usimamizi wa sekta ya madini wenye kuleta tija na manufaa kwa jamii na taifa.
Nyongo aliendelea kusema zebaki iliyopo sasa nchini itaendelea kutumiwa na wachimbaji wadogo wakati huohuo Serikali ikiendelea na juhudi ya kupata teknolojia mbadala na isiyokuwa na madhara kwa mazingira na wananchi itakayo wasaidia wachimbaji wadogo katika uchenjuaji wa madini.
Amesema, serikali inafanya tafiti mbalimbali ili kupata teknolojia mbadala ya uchenjuaji wa dhahabu na pindi itakapopatikana Serikali kupitia vituo vya mfano vilivyopo nchini itatoa elimu ya uchenjuaji kwa njia hiyo ili kuwawezesha wachimbaji wadogo wa madini nchini kupata uelewa wa njia hiyo na hivyo kuachana na matumizi ya zebaki.
Naibu Waziri Nyongo aliongeza kuwa kutokana na utegemezi wa wachimbaji wadogo kwa kemikali hiyo, haiwezekani kusimamisha matumizi yake kwa haraka kwani wengi hujikita kwenye uchenjuaji kwa kutumia kemikali hiyo kunakowawezesha kujipatia kipato na kutunza familia zao.
Aidha, amewaasa wachimbaji wadogo kutumia kemikali hiyo kwa njia salama ili kuepusha athari zitokanazo na kemikali hiyo. Amesema serikali ipo macho kuhakikisha inawaelimisha wachimbaji wadogo namna bora ya matumizi ya kemikali hiyo ikiwa ni pamoja na kuwashauri kutomwaga maji ya zebaki karibu na mito na makazi ya watu ili kuepusha athari zake.
Pamoja na kuzungumzia suala hilo, Naibu Waziri Nyongo alisema ili kuhakikisha kuwa madini yanatutoa watanzania na kukuza uchumi wa nchi na wananchi sharti wafuate taratibu na sheria za nchi.
“Chimba madini, uza madini yako kwenye masoko ya madini, acha kuuza kwa njia za panya, sheria itachukua mkondo wake, tutakukamata, tutataifisha madini, na utapata hasara”. Alisisitiza.
“Ukipata madini lipa kodi lipa tozo fedha hizo ziende kwenye mfuko wa Serikali, Serikali iwekeze kwenye miradi mikubwa ya maendeleo, ijenge shule, ijenge hospitali na barabara, ipende nchi yako. Ukichimba ukashindwa kulipa kodi umeisaliti nchi yako umeusaliti uchumi wa nchi yako”. Alikazia.
Alimalizia mahojiano hayo kwa kuueleza umma wa watanzania kuwa fasheni ya utoroshaji wa madini imepitwa na wakati kwani serikali ina wigo na mkono mrefu hivyo hivyo hakuna atakayejaribu kutorosha madini hayo atakayefanikiwa kwani atakamatwa na atafilisika.