Home Mchanganyiko ULINZI NA USALAMA WAKATI WOTE WA ZOEZI LA KUJIANDIKISHA NA KUPIGA KURA...

ULINZI NA USALAMA WAKATI WOTE WA ZOEZI LA KUJIANDIKISHA NA KUPIGA KURA KUIMARISHWA MKOANI ARUSHA

0

*********************************

Na Ahmed Mahmoud Arusha

JESHI la polisi mkoa wa Arusha,limewahakikishia wananchi kwamba litaendelea kuimarisha ulinzi na usalama  wakati wote wa zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura kwenye  uchaguzi wa serikali za mitaa  zoezi ambalo limeanza Oktoba 8 na litakalohitimishwa Oktoba 17 saa 12 jioni.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Arusha Jonathan Shana, ameyasema hayo leo ofisini kwake mara baada ya kukamilisha ziara ya kuangalia hali ya usalama  kwenye vituo vya kujiandikisha wapiga kura katika jiji la Arusha.

Alisema kuwa jeshi la polisi litaendelea kuimarisha usalama na hivyo kuwezesha wananchi kujiandikisha na kuhakikisha kuwa kipindi chote cha kampeni mpaka uchaguzi na kutangazwa matokeo hakuna matukio ya jinai ambayo yanalenga kuvuruga zoezi hilo.

Kamanda Shana,akisema kuwa amekuta zoezi likiwa limedorora  na hivyo akatoa wito kwa wananchi watumie muda wa nyongeza wa siku tatu uliotolewa na serikali ili waweze kushiriki kujiandikisha  kwenye daftari la wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa ili wawachague viongozi wao .

Kamanda,Shana,alisema serikali imeongeza siku tatu ambapo zoezi hilo lilikuwa lifikie mwisho Oktoba 14 sasa limesogezwa mbele hadi Oktoba 17 saa 12,000 jioni kutokana na kubainika kuwa wananchi wengi walikuwa hawajajitokeza kujiandikisha .

Alisema kuwa jeshi la polisi litaendelea kuimarisha usalama na hivyo kuwezesha wananchi kujiandikisha na kuhakikisha kuwa kipindi chote cha kampeni mpaka uchaguzi na kutangazwa matokeo kutakuwa salama.

 Kamanda,Shana,alisema hadi sasa hakuna tukio lolote la uhalifu ambalo limetokea kwa ajili ya kuvuruga zoezi hilo na kuonya kuwa jeshi la polisi halitasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakae jihusisha na uvunjifu wa amani kwa kufanya makosa ya jinai.

Amesema katika kuhakikisha usalama unaimarishwa jeshi la polisi litatumia vitabu vitatu ambavyo ni kuzingatia kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa za mwaka 2019,mwongozo wa  uchaguzi wa serikali za mitaa pia watazingatia sheria na taratibu za polisi zilizoko kwenye mwongozo wa jeshi hilo yaani PGO ,wakati wote wa kampeni kupiga kura, kutangazwa matokeo.

Alisema wasimamizi wa uchaguzi kwenye halmashauri zote za wilaya katika mkoa wa Arusha watawasilisha ,miongozo,kanuni  na taratibu za uchaguzi kwa wakuu wa polisi wa wilaya OCD ili kuhakikisha kuwa usalama wakati wote wa uchaguzi huo unakuwepo na unaenda bila viashiria vya uvunjifu wa amani.