NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
MAKAMU wa Rais wa Jamhur ya Muungano wa Tanzania ,Samia Suluhu Hassan anatarajia kufungua maonyesho ya viwanda ambayo yanafanyika kwa mara ya pili mkoani Pwani, octoba 17 mwaka huu.
Katika maonyesho hayo ,wenye viwanda 206 wamejitokeza kushiriki .
Maonyesho hayo yataambatana na kongamano la uwekezaji litakalofanyika octoba 19 na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Wazir Mkuu Kassim Majaliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu suala hilo, mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo alisema, waratibu wa maonyesho hayo watakuwa ni wabobezi wa masuala ya maonyesho kama hayo kampuni ya magazeti ya serikali (TSN) pamoja na mamlaka ya maendeleo ya viwanda (TANTRADE) .
Alieleza, malengo ya matukio hayo ni kuonyesha kwamba mkoa wa Pwani ,umedhamiria kuwa ukanda wa viwanda,wenye viwanda kupata masoko ya uhakika,kupanua wigo wa soko la ndani ya mkoa kufikia kimataifa na ,kuvutia wawekezaji wapya.
Aidha Ndikilo alifafanua lengo la kongamano hilo ,kuwa ni kuonyesha fursa za uwekezaji zilizopo mkoani humo kupitia sekta mbalimbali ikiwemo utalii,uchumi,kijamii,kilimo,uvuvi na viwanda.
“Kufanyika kwa kongamano hili italeta picha halisi ya fursa zote zilizopo mkoani Pwani,na kuonyesha namna mkoa ulivyopiga hatua katika sekta ya viwanda,uwekezaji na fursa za miradi mikubwa ikiwemo mradi mkubwa wa ujenzi wa uzalishaji umeme megawatts 2,100 STIGO ,huko Rufiji”alibainisha Ndikilo.
Hata hivyo,mkuu huyo wa mkoa alisema wenye viwanda maonyesho ya mwaka jana walikuwa 166 mwaka huu wanatarajia wameongezeka 206.
Nae Januarius Maganga wa TSN alisema ,wanakwenda kuratibu maonyesho hayo ikiwa ni maonyesho ya kumi .
Maonyesho hayo pia yatafungwa octoba 23 mwaka huu na Wazir Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda