Home Mchanganyiko MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA MWANAMKE KIJIJINI KUFANYIKA OKTOBA 15...

MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA MWANAMKE KIJIJINI KUFANYIKA OKTOBA 15 MWAKA HUU

0

Tarehe 14 Oktoba 2019.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii) inataarifu umma na wadau kwa ujumla kuwa Tarehe 15 Oktoba ya kila mwaka Tanzania inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mwanamke anayeishi Kijijini.

Maadhimisho haya hufanyika kila ifikapo tarehe 15, Oktoba kufuatia Tamko la Umoja wa Mataifa kwa kwa mujibu wa Azimio Namba 62 la Tarehe 18 Disemba, 2007. Azimio hilo lilitambua Tarehe 15 Oktoba, kila mwaka kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Wanawake Wanaoishi Vijijini na kuzitaka Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuadhimisha Siku hiyo.

Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI, wanawake, wanaume na wadau wanaotoa huduma vijijini inatarajia kufanya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mwanamke Anayeishi Kijijini, kuitikia dhamira ya kuungana na Nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa. Kimataifa, Maadhimisho haya yalifanyika kwa mara ya kwanza tarehe 15 Oktoba, 2018.

Lengo la Maadhimisho ni kutambua na kuuenzi mchango wa wanawake wanaoishi vijijini hususan katika nyanja za uzalishaji wa mazao ya Kilimo, kuhakikisha Usalama wa Chakula Kaya na kuchangia Ukuaji wa Uchumi wa Taifa.

Nchini Tanzania, Maadhimisho yatafanyika kwa mara ya Pili na Kaulimbiu ya mwaka 2019 iliyotolewa na Umoja wa Kimataifa kwa lugha ya Kiingereza ni “Rural Women and Climate Resilience”, ambayo imetoholewa na kuwa na Kaulimbiu ya Kitaifa isemayo “Tuwekeze Kwa Wanawake Wanaoishi Vijijini, Kukabiliana na Mabadiliko Ya Tabianchi”.

Ufafanuzi wa Kaulimbiu ya mwaka 2019 unaitaka jamii na wadau kuzingatia Athari za Mabadiliko ya Tabianchi zinazowakabili zaidi wananchi wanaoishi vijijini ambao wanajishughulisha na Kilimo kinachotegemea mvua.

Kaulimbiu inasisitiza umuhimu na nafasi kubwa ya Wanawake wanaoishi vijijini katika kushughulikia athari hizo, ambazo ni pamoja na Ukame, Mafuriko na Njaa mambo amabyo ni baadhi ya matokeo yanayoongeza ugumu wa maisha kwa wanawake wanaoishi vijijini.

Serikali inatambua kuwa mila na desturi zina nguvu katika jamii zinazoishi vijijini, kwa kiwango kikubwa baadhi zina hitilafu kwani zinawakandamiza wanawake kwa kuweka masharti katika mgawanyo wa majukumu na Rasilimali ya Familia. Baadhi ya masharti huwekwa katika Vyakula vyenye Lishe bora, Malezi ya Watoto na Utamaduni unaoweza kuchangia katika Vitendo vya Ukatili wa Kijinsia.

Wanawake wanaoishi vijijini ni Wakala wazuri wa kuleta mabadiliko katika jamii kwa kuwa wanajukumu la Malezi ya Watoto ambao huleta uendelevu wa Vizazi na Uwekezaji katika masuala ya Usalama wa Chakula na Afya ya Familia kwa kuzingatia usafi wa mazingira, Lishe bora na kuhudumia wagonjwa katika familia.

Maadhimisho ya mara ya kwanza hapa Nchini yalifanyika katika Kijiji cha Manchali B kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino katika mkoa wa Dodoma.

Katika kumwezesha mwanamke anayeishi kijijini Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuboresha Miundombinu ya Vijijini kupitia, Taasisi zake za SIDO, REA,TARURA na Vitambulisho vya Ujasiriamali ikiwa ni hatua za kuwezesha wananchi kiuchumi. Jitihada hizi zimeelekezwa kwa Wanawake waishio vijijini ambao ni nguvu kazi ya Uzalishaji wa mazao ya Kilimo, uhakika wa Chakula katika Kaya, shughuli za kujipatia kipato/kiuchumi na Walezi wa Familia kwa ajili ya uendelevu wa vizazi.

Pamoja na jitihada hizi bado zipo changamoto kama vile Miundombinu hafifu, ushindani katika masoko, upungufu wa Vitendea kazi na Teknolojia sahihi za kurahisisha kazi, kuongeza Ubora wa bidhaa, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Asasi za Kiraia kutoa huduma Mjini zaidi kuliko Vijijini.

Maadhimisho haya hutumika kuunganisha Wadau, kushirikisha Wanawake katika Mtandao wa kibiashara na pia kusaidiana, kutafuta Vitendea kazi vya kurahisisha kazi maeneo ya vijijini na Teknolojia sahihi za uzalishaji ili kuongeza Ubora na kumudu Ushindani wa kibiashara katika Soko.

Shughuli zinazofanyika katika Wilaya ya Hanang ni Ufugaji, Kilimo cha Nafaka na Ujasiriamali. Maadhimisho haya yanatarajia kuleta mabadiliko katika maeneo yafuatayo:
Mosi ni kuongeza uelewa na elimu kwa umma kuhusu fursa zilizopo na jitihada za Serikali katika uwezeshaji wa wanawake kiuchumi kupitia mada zitakazowasilishwa na wataalamu katika viwanja vya kijiji cha Gehandu, Halmashauri ya Hanangi katika Mkoa wa Manyara.

Pili ni kutekeleza kwa vitendo Mkakati ya kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Tabianchi kwa kuhifadhi Mazingira kwa ajili ya Uhai wetu na Vizazi vijavyo;
Tatu Ukusanyaji wa Takwimu za hali iliyokuwepo na mabadiliko chanya yanayojitokeza katika Maendeleo na Ustawi wa jamii husika baada Maadhimisho.

Mwisho napenda kutoa pongezi kwa Wadau na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ambayo yanatoa Huduma kwa wananchi wanaoishi maeneo ya Vijijini. Wizara inatoa wito waendelea kushirikiana na Serikali katika ngazi zote ili kutoa Huduma kwa Uwazi na kuweka utaratibu utakaosaidia kuondoa udhaifu katika kukuza ustawi na maendeleo ya wanawake na jamii kwa ujumla, Na dhamira hii itatekelezwa kwa umakini kutegemea upatikanaji wa takwimu na taarifa sahihi kuhusu mahiatji ya jamii zetu.