Home Mchanganyiko HAZINA SACCOS KUWEKEZA MRADI WA BILIONI 52 DODOMA

HAZINA SACCOS KUWEKEZA MRADI WA BILIONI 52 DODOMA

0

Mwenyekiti wa Bodi wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Hazina Saccos,Bw. Aliko Mwaiteleke akifafanua jambo mbele ya Wanachama  waliohudhuria mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama hicho uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano Hazina, leo jijini Dar es Salaam.

***********************

Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam

CHAMA cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Hazina Saccos kimeazimia kujenga kitega uchumi cha kisasa kwa gharamaya  Shilingi bilioni 52 kupitia mradi wa Njedengwa katika Jiji la Dodoma ili kukuza uchumi wa mkoa wa Dodoma na Taifa kwa kupitia kodi.

Hayo yamebainishwa leo Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi wa chama hicho cha Ushirika Bw. Aliko Mwaiteleke  wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka  uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano Hazina,  na kuongeza kuwa mradi huo upo katika hatua za mwisho za utekelezaji wake.

Mwaiteleke alisema mpaka sasa upembuzi yakinifu wa mradi huo utakaojengwa kwa njia ya ubia kati ya Hazina Saccos na mwekezaji kwenye neo lenye ukubwa wa ekari 22  kupitia utaratibu wa Jenga, Endesha na Hamisha (Build, Operate and Transfer – BOT) ambapo mwekezaji atagharamia ujenzi wote na kuendesha kwa muda ambao utakubaliwa ndani ya mkataba.

Alisema mradi huo unasimamiwa na Kamati ya watu Saba wakiongozwa na Profesa Esta Eshengoma kutoka Chuo Kiuu Cha Dar es Salaam na wajumbe wake kutoka Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru),  Bodi ya Manunuzi ya Umma (PSPTB), Kituo Cha Uwekezaji (TIC), na Chuo Kikuu cha Ardhi ambao kwa sasa wanafanya kazi ya kusaka mwekezaji ili kufanikisha mradi huo.

Bw. Mwaiteleke alifafanua kuwa Mradi wa Njedengwa upo mbioni kuanza  na unategemewa kuwa chachu ya maendeleo ya chama hicho kwa kukiingizia kipato kutokana na shughuli zitakazokuwa zikifanyika kupitia mradi huo.

Alifafanua kuwa  mradi huo utahusisha ujenzi wa hoteli ya kisasa, kumbi za  mikutano, majengo ya Ofisi,  Viwanja vya Michezo na bwawa maalum la kuogelea.

Aidha alisema Chama hicho cha Hazina Saccos ambacho kina wanachama 5,600 kina mtaji mtaji wenye thamani ya shilingi bilioni 10 ikiwa ni fedha taslimu na mali wanazozimiliki ikiwemo ardhi ambazo zimekuwa na manufaa makubwa kwa wanachama..

“Mwaka jana pekee kupitia akiba na mikopo  tulipata faida ya shilingi milioni 64 na kila mwanachama alipewa gawio la asilimia 20 kulingana na hisa zake”alisema Mwaiteleke.

Alisema faida nyingine waliyopata kupitia Hazina Saccoss ni kununua viwanja 150 katika maeneo mbali mbali ya mkoa wa Dar es Salaam na Pwani na kuwakopesha wanachama wao kwa bei nafuu ambapo wanalipa kidogo kidogo kwa miezi 60.

“Pia Dodoma tumenunua viwanja 897 katika maeneo ya Ihumwa Ngaloni, Iyumbu  (maeneo ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ambavyo tumevigawa kwa wananchi na viwanja vya Nzuguni tutaanza kuvigawa baada ya taratibu za Halmashauri ya Jiji la Dodoma kukamilika ili kuwawezesha wanachama wetu waliohamia Dodoma kupata maeneo ya kujenga makazi yao” alisema Bw. Mwaiteleke

Naye Meneja wa Hazina Saccos Bw. Festo Mwaipaja, alisema Saccoss hiyo sio ya wafanyakazi wa Wizara ya Fedha peke yake bali watumishi wote wa serikali wanaruhusiwa kujiunga na chama hicho isipokua vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo ni jeshi, Polisi, na Usalama wa  Taifa.

Alisema kwa mtumishi wa umma kujiunga na chama hicho cha ushirika mbali na kuwa muajiriwa pia atapaswa kulipa kingilio cha shilingi 20,000 na kununua hisa kuanzia 20 ambazo kila hisa moja ni shilingi 10,000 na kufanya thamani ya hisa zote kuwa shilingi 200,000.

Aidha alisema kuna mchango wa shilingi 20,000 kila mwezi na kuwataka watumishi wa umma kutoka taasisi na idara zote za serikali kuchangamkia fursa ya kujiunga na ushirika huo ili kujiinua kiuchumi

Kuhusu viwanja, Bw. Mwaipaja alieleza kuwa Chama hicho kimetumia zaidi ya shilingi bilioni 4 kununua viwanja katika Jiji la Dodoma na kuchangia eneo hilo kuwa na mzunguko mkubwa wa fedha kwa wenyeji na kwamba hayo ni mafanikio yanayoihusu jamii.

Akifungua Mkutano Mkuu huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Mary Maganga, ameipongeza Hazina Saccos kwa kuwapatia viwanja wanachama wake na kuwataka wanachama waliopata fursa ya kupata viwanja hivyo waviendeleze haraka ili kuodokana na changamoto ya malazi kwa kuwa baadhi walipata viwanja hivyo tangu mwaka uliopita, 2018.

Aidha, ameipata kongole Hazina Saccos kwa hatua waliyofikia ya kutafuta mwekezaji katika mradi wa Njedengwa ambao utaongeza mapato ya Ushirika na kuwataka viongozi na wanachama kuhakikisha wanazingatia taratibu Sheria na Kanuni ili kufanikisha mradi huo muhimu.