MKUU wa wilaya ya Mpwapwa Jabir Shekimweri amefanya ziara mtaa kwa mtaa kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha katika daftari la orodha ya wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika novemba 24 mwaka huu.
Mbali na kuhamasisha wananchi kujiandikisha,ametumia ziara hiyo pia kujiandikisha yeye mwenyewe katika kituo cha National.
Akizungumza na wananchi mbalimbali katika ziara hiyo,Shekimweri amewahimiza kutumia siku tatu zilizoongezwa vizuri ili kila mtu aweze kushiriki zoezi hilo.
“Zoezi hili ni letu sote,halipaswi kupuuziwa,kila mmoja ajione ana wajibu wa kushiriki ili mradi awe na umri wa kuanzia miaka 18,tuhimizane,tukumbushane na tuelimishane,”alisisitiza mkuu huyo.
Amesema maendeleo yoyote yanaanzia ngazi ya kijiji hivyo ni wajibu wa wananchi kujiandikisha ili wapate fursa ya kuchagua viongozi waadilifu na wenye kasi kama ya Rais John Magufuli.
“Kuna watu wana sema tayari Rais Magufuli yupo anafanya kazi nzuri inatosha,hapana ili Rais wetu afanye kazi nzuri zaidi anahitaji kuwa na wasaidizi huku chini watakaoibua changamoto zenu na kuziwasilisha juu ili zifanyiwe kazi,na watu hao ndio viongozi watakaochaguliwa novemba 24,”aliongeza Shekimweri.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wamemuhakikishia mkuu huyo kuendelea kutoa elimu ili wajitokeze kujiandikisha.
“Mimi hapa nimeshajiandikisha, na nimpongeze Rais Magufuli na wewe mkuu wa wilaya kwa kazi mnayoifanya,lakini sisi wananchi hatupaswi kuridhika na nyinyi tu viongozi wetu lazima tujiandikishe ili tuchague viongozi wa mitaa na ndio mafanikio ya serikali ya awamu ya tano hasa tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa 2020,”alisema Boniface Mapuya.
Joyce Chikolo mkazi wa Mpwapwa mjini amewasihi wananchi wenzake kujiandikisha ili wapige kura kuchagua viongozi wao.
“Kuna watu hapa wakati wa kujiandikisha hawatoki,hivyo na kura hawapigi,siku wanapatwa na shida hata mwenyekiti wao wa mtaa au kijiji hawamjui,jamani twendeni mkajiandikishe,”alisema Joyce.
Zoezi la uandikishaji awali lilikuwa lihitimishwe octoba 14 lakini kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI)Selemani Jafo inasema zoezi hilo limeongezwa muda wa siku 3 hivyo litafikia tamati octoba 17 mwaka huu.