Home Mchanganyiko DC KATAMBI AONYA WANAOWAKATISHA MASOMO WATOTO WA KIKE

DC KATAMBI AONYA WANAOWAKATISHA MASOMO WATOTO WA KIKE

0

Na.Alex Sonna,Dodoma

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi amewaonya watu wenye tabia ya kuwapa mimba au kuoa watoto waliochini ya miaka 18, akisema sheria ni kali itachukuliwa pia kwa wazazi ambao wanalazimisha watoto wao kuolewa kabla ya wakati.

Ameyasema hayo leo Jijini hapa katika  Shule ya Sekondari ya Mnadani wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike,  Katambi amesema hatokubali kuona binti yeyote anashindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya kuolewa au kupata mimba kabla ya wakati ndani ya Wilaya anayoiongoza.

” Serikali ya awamu ya tano ya Rais Magufuli inapiga vita sana vitendo vya kinyanyasaji vinavyofanywa dhidi ya mtoto wa kike, ni rai yangu kwa jamii zetu kwa ujumla kuilinda haki ya mtoto wa kike isipotee na Mimi stakubali kuona vitendo hivi ndani ya Wilaya yangu”amesema Dc Katambi.

Kama Mkuu wetu wa Nchi ametoa nafasi nyingi za kiuongozi kwa wanawake basi ni jukumu letu kuhakikisha watoto wetu wa kike wanapata elimu bora ili kuja kuitumikia nchi yao katika nafasi mbalimbali, 

Ameonya vitendo vya mila  potofu kwa watoto wa kike hasa kwa kukubali kuwaoza wakiwa bado wanafunzi pamoja na kuwafanyia vitendo vingine vya kikatili ikiwemo ukeketaji kwani vitendo hivyo havikubaliki kabisa.

Amesema ili kuwa na taifa imara lenye uchumi wa kati kupitia viwanda ni lazima pia kukubali kuwanyanyua wanawake na kutupilia mbali mila na tamaduni ambazo hazina tija kwa watoto wa kike.

“Sheria zipo wazi kabisa ole wenu ukutwe na mwanafunzi wa kike, uwe ni Mwalimu, Mfanyabiashara, Mtumishi wa Serikali au bodaboda tutahakikisha tunakuchukulia hatua kali za kisheria, yeyote tutakayemkamata atakua mfano kwa wengine, ” Amesema DC Katambi.

Amewataka walimu na wanafunzi kushirikiana kutoa taarifa kwenye vyombo vya sheria wanapobaini  kuna vitendo vya unyanyasaji na ukandamizaji wanavyofanyiwa watoto wa kike hasa wanafunzi.