Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Tulia Ackson amefanya ziara ya kuwatembelea na kuwapa pole wafiwa waliopoteza ndugu zao kwenye ajali ya daraja linalounganisha kata za Mwasanga na Tembela Mkoani Mbeya kufuatia mvua kubwa iliyosababisha daraja hilo kuvunjika siku nne zilizopita na kusababisha vifo vya watu wanne waliokuwa wakivuka katika daraja hilo.
Akiongozana na baadhi ya Viongozi wa Serikali akiwemo Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya ACP James Kasusura, Diwani wa Kata ya Mwasanga Mhe. Hokola pamoja na viongozi wa CCM, Dr. Tulia ametoa misaada mbalimbali kwa wafiwa ikiwemo kilo 100 za Mchele, kilo 40 za Maharage pamoja na pesa Taslim Shilingi 600,000/- (huku taasisi ya Tulia Trust ikichangia jumla ya Shilingi 200,000/-)
Akizungumza na Wananchi hao Dr. Tulia amesema “Tumepoteza ndugu zetu katika jambo hili baya lililotupata, nilizipata taarifa hizi nikiwa safarini, nimerejea leo na nimeona nije niwaone ndugu zangu kwa hili janga lililotupata. Niwashukuru sana Wanajamii kwa kujitoa kwenu katika kuendelea kuwafariji wenzetu hawa waliopoteza ndugu zao.”
Pia Dr. Tulia amesema “kikubwa zaidi niwapongeze na kuwashukuru Serikali ya Mkoa ikiongozwa na Mhe. Albert Chalamila pamoja na Jiji kwa hatua kubwa ambazo wamekwisha chukua hadi sasa hivi. Kwa wakati huu hatua ya awali ilikuwa ni kuwahifadhi kwanza Marehemu ambao wamepoteza maisha kwenye hili janga na pia wametoa michango mingine ya chakula na fedha kwa ajili ya kuwasaidia hawa wenzetu wafiwa.”
Wakati huo huo ametoa rai kwa jamii kukaa na watoto kwa ukaribu katika kipindi hiki cha mvua. Amesema “mvua ni nyingi na maji ni mengi kwahiyo mtoto mdogo anaweza asijue maji ni mengi kiasi gani hivyo tuendelee kukaa nao karibu ili kuepukana na hizi changamoto”-Dr. Tulia