************************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza watendaji katika ngazi zote wahakikishe kuwa vijana wanawezeshwa kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Oktoba 10, 2019) wakati akizindua maadhimisho ya wiki ya vijana kitaifa mwaka 2019 kwenye viwanja vya Mpilipili, nje kidogo ya mji wa Lindi.
“Vijana tushirikiane na Serikali na kufanya kazi kwa bidii ili kuunga mkono jitihada za Serikali yetu ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwaletea wananchi maendeleo. Hatua hii itatuwezesha kama Taifa tuvuke na tufikie uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025,” amesema.
Amesema wakati anatembelea mabanda ya maonesho, ameona ubunifu wa kijana ambaye ameunda mashine ya kumsaidia mtoto njiti apate joto na pia amemuona kijana mwingine ambaye amebuni mtambo wa kupukuchua magunia 100 ya mahindi kwa saa.
Pia alitembelea banda la kikundi cha vijana kutoka China, Korea Kusini, Argentina, Arzebhaijan na Tanzania ambao waliishi kwenye mazingira magumu na wakabadilika na wameamua kushiriki maonesho hayo ili kuwabadilisha mtazamo vijana wenzao.
“Nimefurahi kuwaona hawa vijana, ninaamini watashirikiana na wenzao wa hapa kuwabadilisha vijana wa Tanzania ili wawe na fikra endelevu.”
Akizungumzia mikakati ya kuwawezesha vijana kiuchumi, Waziri Mkuu amesema Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini, imeanza kutoa mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba (greenhouse) katika mikoa yote na Halmashauri zote nchini.
Amesema teknolojia hiyo itawasadia wakulima kupata mazao mengi katika eneo dogo na kupata mazao bora yanayokidhi viwango katika soko la ndani na nje ya nchi. “Kwa kutumia teknolojia hii, vijana wengi watapata ajira katika sekta ya kilimo,” amesema.
Waziri Mkuu amesema mkakati huo ni utekelezaji wa agizo la Chama cha Mapinduzi ambacho kinatambua kuwa sekta ya kilimo ndiyo kimbilio la wananchi walio wengi na kupitia ilani yake ya mwaka 2015 Ibara ya 6 (a) imeielekeza Serikali “kuwawezesha wakulima kupata mafunzo ya kilimo cha kisasa, pembejeo, zana za kisasa na wataalamu wa ugani pamoja na mbinu za kuyafikia masoko ya uhakika ya mazao yao”.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeziagiza Halmashauri zote nchini zitenge maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za vijana ikiwa ni pamoja na maeneo kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vinavyomilikiwa na vijana.
“Kwa mujibu wa taarifa tulizonazo, hadi mwishoni mwa mwaka jana, zaidi ya ekari 217,882.36 zilikwishatengwa. Ninaziomba Halmashauri zote zisimamie na kutekeleza agizo hilo ili kuhakikisha maeneo hayo yanatumiwa kama ilivyokusudiwa,” amesema.
Moja ya shughuli zitakazofanyika wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Vijana mwaka huu ni kuwa na kongamano la vijana linalojumuisha nchi za Afrika Kusini, Zimbabwe, Msumbiji, Kenya, Uganda na Angola. Miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa ni mchango wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere katika maendeleo ya Afrika; Mabadiliko katika elimu na ukuzaji ujuzi kuelekea uchumi wa kipato cha kati ifikapo 2025; na Matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kuelekea uchumi wa viwanda.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wananchi waliohudhuria uzinduzi huo, Waziri wa Nchi OWM – Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Bi. Jenista Mhagama alisema sambamba na maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa Programu ya kukuza ujuzi nchini ambayo imelenga kutoa mafunzo ya stadi mbalimbali za kazi kwa vijana wa ngazi mbalimbali.
“Mpaka sasa, vijana wapatao 32,736 wameshapata mafunzo na mwaka huu, Ofisi ya Waziri Mkuu vijana wengine 46,000 watapata mafunzo mbalimbali ikiwemo kilimo cha kisasa,” alisema.
Naye, Waziri wa Vijana, Sanaa, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Ally Abeid Karume amewataka vijana kote nchini washikamane kwenye shughuli zao za uzalishaji mali na pia amewasisitizia haja ya kuwa wazalendo.
“Vijana mnategemewa kuwa wazalendo. Kuna tofauti kati ya kuwa raia na kuwa mzalendo. Uraia unaupata kwa kuzaliwa na uzalendo unaonekana kwa vitendo na hasa kwa kuwa na maadili mema,” alisema.
“Pia vijana mnategemewa muendelee kuwa wachapakazi. Naomba msonge mbele zaidi na mfanye kazi kwa bidii ili muweze kumudu ushindani katika mataifa ambayo yako mbele kiteknolojia zaidi yetu. Serikali zenu zote mbili zitaendelea kuunga mkono shughuli za vijana za uzalishaji wa bidhaa zenye ubora wa kimataifa.”