********************************
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
SERIKALI Mkoani Pwani, imetoa rai kwa wananchi kupuuza baadhi ya watu wanaowahadaa kuwa kitambulisho cha Taifa -NIDA na cha kupiga kura wataweza kupigia kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa,vitongoji na vijiji Novemba 24 mwaka huu,suala ambalo ni upotodhaji mkubwa.
Aidha imeweka bayana takriban watu 680,000 wanatarajiwa kujiandikisha kwenye daftari hilo, hivyo wamehamasishwa kujiandikisha ili kuwa na haki ya kupiga kura kuchagua viongozi wanaowataka.
Akihamasisha umuhimu wa kujiandikisha katika daftari hilo hadi octoba 14 mwaka huu ,wakati alipokwenda kutimiza haki yake ya msingi kujiandikisha kituo cha Mwanalugali ‘A ‘ Kibaha ,mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo alisema kitambulisho cha Taifa na cha kupigia kura havitahusika katika zoezi la kupiga kura.
“Nimetumia haki yangu ya msingi kujiandikisha ,nimejiandikisha wa 123 lengo la kituo hiki ni kuandikisha watu 1,332, na kimkoa tunatarajia kuwa na watu 680,000 ,alifafanua Ndikilo.
“Wapo baadhi ya watu wanahadaa wenzao kwamba hakuna ulazima wa kujiandikisha kwenye daftari la wakazi ,na badala yake watatumia vitambulisho kama si cha uraia basi cha kupiga kura,sio kweli mtapoteza haki yenu ya msingi”
Hata hivyo Ndikilo alieleza ,suala la kupiga kura ni la wananchi wote siyo la watu wachache ili kuondoa malalamiko kuwa viongozi waliochaguliwa hawafai wakati wao hawakushiriki hilo ni tatizo.
Alisema taratibu zote zimekamilika ikiwa ni pamoja na fedha ambapo wasimamizi tayari wameshateuliwa kwa ajili ya uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 24 mwaka.
Katika hatua nyingine ,anaeleza ni wakati wa mabadiliko na kujitambua kuacha kuchagua viongozi wanaokingiwa kifua na fedha zao kutoa rushwa bali wachague viongozi walio bora ,watakaowaletea maendeleo.
Nae ofisa uchaguzi wa halmashauri ya Mji wa Kibaha ,Saidi Kayangu alisema ,wamejipanga kuweka mazingira rafiki na kusimamia haki kwa makundi yote ili kuondoa vikwazo wakati wa uchaguzi.
Alitoa wito kwa wananchi wenye sifa kushiriki katika uchaguzi huo muda utakapowadia kwani ushiriki wao ndio mchango katika maamuzi na washiriki bila rushwa.
Kayangu alihimiza, wananchi kujiorodhesha kwenye rejesta za wakazi katika mitaa yote 73 ili kupata takwimu kwa uhalisia hasa idadi ya kuanzia umri wa miaka 18 na kuendelea,:”hatua hii anaelezea itasaidia maandalizi ya uchaguzi kama vile idadi ya karatasi za kupiga kura.