Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud akieleza thamani ya Mwanamke wakati akifunga Kongamano la siku mbili la mthamini Mwanamke huko katika Ukumbi wa Manispaa Magharibi “A”
Mwenyekiti wa chipkizi wa Mkoa wa Magharibi kichama Rukaiya Maktuba Haji akielezea jinsi alivopata mafunzo ya mthamini Mwanamke katika Kongamano la siku mbili katika Ukumbi wa Manispaa Magharibi “A”
Baadhi ya washiriki waliohudhuria katika ufungaji wa Kongamano la siku mbili la mthamini Mwanamke katika Ukumbi wa Manispaa Magharibi “A”
Picha na Maryam Kidiko – Maelezo Zanzibar.
…………………………
Na Mwashungi Tahir,Maelezo
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud amesema mwanamke ni kiumbe mwenye thamani na anastahiki kuenziwa na kupewa thamani yake katika jamii.
Akifunga Kongamano la Mthamini Mwanamke kwa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Magharibi kichama katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa Wilaya ya Magharibi “A” huko Kianga amesema mwanamke anathamani kubwa kwani hata vitabu vya dini vimempa hadhi na daraja yenye kuheshimika.
Amesema mwanamke ana fursa kubwa ya kuleta maendeleo kwa taifa kupitia michango yao, busara , hekima na malezi bora hivyo amewasisitiza kujiendeleza kielimu na kujitokeza katika kugombea nafasi mbali mbali za uongozi.
“Mwanamke ni mtu mwenye thamani kubwa katika jamii na anapaswa kuheshimika kwani ni mama zetu ambao wamejaaliwa busara kubwa wakiwepo sehemu yeyote ya maendeleo “, alisema Mkuu huyo.
Mhe. Ayoub alieleza Zanzibar imeweka sheria katika kuwalinda wanawake na watoto katika kupata haki zao za msingi hivyo jamii inapaswa kumthamini mwanamke katika na hadhi yake anayostahiki.
Aidha amekemea tabia ya kumdharau wanamke na kumwona kuwa hana hadhi katika jamii na kumfanyia vitendo vya udhalilishaji ikiwemo kupigwa na waume zao, kuwakosesha elimu, kutelekezwa na watoto kufanya hivyo ni kinyume na sheria na kuhakikisha kuwa atasimamia vyema suala zima la udhalilishaji nchini.
Nao washiriki wa kongamano hilo wamesema wataelimisha jamii kuhusu thamani ya mwanamke ili aweze kutambulika na kuheshimika ili kuweza kutokomeza kabisa vitendo vya udhalilishaji nchini.
Kongamano hilo la siku mbili ambalo limewashirikisha vijana mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi wa Mkoa wa Magharibi mada mbali mbali zimejadiliwa ikiwemo mwanamke na uongozi, Udhalilishaji na Athari za mimba za utotoni.