Home Mchanganyiko NDITIYE: MAWASILIANO YATUMIKE KUPUNGUZA MAAMBUKIZI YA UKIMWI

NDITIYE: MAWASILIANO YATUMIKE KUPUNGUZA MAAMBUKIZI YA UKIMWI

0

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye akisisitiza jambo kwa viongozi wa kampuni za simu za mkononi (hawapo pichani) wakati wa kikao akiwa ziarani Mkoani Mwanza. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dkt. Philis Nyimbi

Mkuu wa Kanda ya Ziwa wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Mhandisi Francis Mihayo akitoa taarifa kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (aliyeketi mbele katikati) kabla ya kuzungumza na wawakilishi wa kampuni za simu za mkononi wa mkoa wa Mwanza akiwa ziarani mkoani humo

Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Mwanza na Simiyu wa Halotel, Ismail Msami akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (mwenye fulana ya kijani) wakati wa kikao chake na kampuni za simu za mkononi akiwa ziarani mkoani Mwanza

Mbunge wa Jimbo la Nyamagana akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhamasisha usajili wa laini za simu wakati wa kikao cha Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (hayupo pichani) na kampuni za simu mkoani Mwanza

…………

Na Prisca Ulomi, Mwanza

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amezitaka kampuni za simu za mkononi kuweka ujumbe au tangazo kwenye simu za wateja kwa lengo la kuendesha kampeni ya kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI kwa wananchi

Nditiye ameyasema hayo akiwa kwenye kikao na viongozi wa kampuni hizo mkoani Mwanza na kuwataka watengeneze na kuweka ujumbe au tangazo hilo kuanzia tarehe 15 Oktoba mwaka huu hadi Siku ya Kilele cha Maadhimisho ya Ugonjwa wa UKIMWI yanayofanyika tarehe mosi Novemba kila mwaka ambao utawakumbusha wananchi kuwa UKIMWI bado upo, ni janga la kitaifa na hauna dawa

“Ninyi ni mawasiliano na mawasiliano yananihusu, sisi tunapatikana kila dakika kuliko televisheni, redio au magazeti, kila mwananchi anapatikana kwa kuwa ana simu ya mkononi na ninyi mtusaidie kutangaza masuala ya kimkakati ya kitaifa mfano janga la UKIMWI bado lipo, mtusaidie kuweka ujumbe kuhusu ugonjwa huu ili tusaidie wananchi,” amesema Nditiye

“Ikilazimika mtume hata ujumbe kuhusu ugonjwa huu ili ujumbe huo uanze kusikika kwa kuwa watanzania ni wateja wenu wakubwa tuwahudumie na wenye simu wengi ni watu wenye uwezo na kwa bahati mbaya ndio wanaopatwa na majanga ya magonjwa haya na hao ndio wateja hivyo tuwasaidie,” amesisitiza Nditiye

Mkuu wa Kanda ya Ziwa wa Vodacom, Gwamaka Mwakilemba amemweleza Nditiye kuwa wako tayari kuandaa ujumbe au tangazo hilo kwa kuwa janga la UKIMWI linagusa jamii ambayo ni wateja wa kampuni yao

Pia, ameiomba Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuongeza kasi ya kutoa namba au vitambulisho vya taifa ili kampuni za simu ziweze kusajili wananchi kwa kuwa wananchi wako tayari kusajili laini zao za simu za mkononi kwa alama ya vidole kwa kuwa wanaogopa kufungiwa laini zao ifikapo tarehe 31 Desemba mwishoni mwa mwaka huu

Naye Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Stanslaus Mabula ameziomba kampuni za simu za mkononi kuwa sehemu ya kupiga vita maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI na kutoa tahadhari kwa wateja wake kupitia ujumbe kwenye simu zao. Pia, ametoa rai kwa wananchi wote nchini kujitokeza kusajili laini zao za simu za mkononi na wasisubiri mpaka siku za mwisho kusajili bali wajisajili kwa wakati ili kuepusha usumbufu na changamoto siku za mwisho

Mabula amewaomba NIDA kuongeza watumishi wa kutosha kutoa vitambulisho vya taifa na amewaomba wabunge wenzake kuhamasisha wananchi na kuwaelimisha kusajili laini zao kwa alama za vidole kwa kuwa tukiwasiliana tunachangia uchumi wa taifa letu ili kufikia uchumi wa kati  

Wawakilishi wa kampuni za simu za mkononi wamemshukuru Mkuu wa Kanda ya Ziwa wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Mhandisi Fracis Mihayo kwa kuwaweka pamoja kampuni za simu za mkononi kama washindani na wapinzani wa kibiashara kwa lengo la kufanikisha kusajili laini za simu za mkononi kwa alama za vidole

Nditiye amewapongeza kampuni za simu kwa kuitikia wito wa Serikali wa kusajili laini za simu za wananchi kwa alama za vidole. Pia amewaomba kampuni hizo kuwaelewesha mawakala wao kuwa wasiwanyanyase wananchi na wasiwatoze kusajili laini zao kwa kuwa usajili wa laini ni bure na wananchi hawapaswi kulipa gharama yeyote