Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Dkt. Tulia Ackson akisalimiana na Rais wa Shirika la Msalaba Mwekundu (TRCS), Ndugu David Kihevile wakati alipowasili kwa ajili ya kufungua Mkutano Mkuu wa Taifa wa Shirika hilo uliofanyika katika Ukumbi wa Royal Village wa Jijini Dodoma.
Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Dkt. Tulia Ackson akifungua Mkutano Mkuu wa Taifa wa Shirika la Msalaba Mwekundu (TRCS) uliofanyika katika Ukumbi wa Royal Village wa Jijini Dodoma.
***********************
Debora Sanja, BUNGE.
Naibu Spika, Mhe. Dkt. Tulia Ackson amelishauri Shirika la Msalaba Mwekundu (TRCS) kufungua matawi mengi zaidi na imara yenye wanachama wa kutosha ili huduma wanazozitoa ziwafikie watu wengi zaidi.
Naibu Spika alitoa ushauri huo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Taifa uliofanyika katika Ukumbi wa Royal Village Jijini Dodoma.
Alisema matawi hayo yatasaidia kutoa elimu khusiana na Shirika hilo kwa wananchi wengi zaidi ili waweze kujua majukumu ya Shirika na vilevile kuwajengea uzalendo na jinsi ya kufanya shughuli za kujitolea.
“Niwapongeze pia kwa kuanzisha Baraza la Vijana , niwatie moyo wa kuendelea na mkakakti wenu wa kuwashawishi vijana wengi zaidi wajiunge na taasisi yenu kupitia klabu za vijana mashuleni, vijana ndiyo nguvu kazi ambayo ikitumiwa vizuri basi mtachangia kujenga jamii bora yenye kuwajibika na kufanya kazi kwa bidii,” alisema.
Aidha, alilitaka Shirika hilo kuzingatia Kanuni zao za kibinadamu, uadilifu, kutopendelea, uhuru, kujitolea, umoja na ushirikiano.
“Kwa kufanya hivyo mtakuwa mnajenga Taasisi imara ambayo inaaminiwa na kuheshimika mbele ya Serikali, wadau mbalimbali na jamii kwa ujumla,” alisema
Alisema Bunge limeifanyia marekebisho mara kwa mara sheria iliyoanzisha Shirika hilo ili kuipa nguvu na kuliwezesha kutimiza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa na kwamba Bunge lipo tayari kuendelea kushirikiana na Shirika hilo.
Katika Mkutano huo Naibu Spika alikubali ombi la kuwa Balozi wa Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania na kuahidi kuifanya kazi hiyo kwa uaminifu na unyenyekevu mkubwa.
Awali Rais wa Shirika hilo, Ndugu David Kihevile alimshukuru Naibu Spika kwa kukubali kuwafungulia Mkutano wao .
Alieleza majukumu ya Shirika hilo kwamba ni kutoa huduma mbalimbali za kibinadamu na kwamba Shirika hilo lingetamani kila Mtanzania awe na moyo wa ubinadamu wa kusaidia jamii ya watu wanyonge.
Katika Mkutano huo Naibu Spika alitunikiwa uanachama wa Shirika la Msalaba Mwekundu.