Katibu Msaidizi Ajira na Nidhamu, Tume ya Utumishi wa Umma Bi. Celina Maongezi akiwasilisha mada, wakati wa kikao kazi kati ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb), Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma na Watumishi wa Mkoa wa Simiyu kilichofanyika katika Shule ya Msingi Bariadi Alliance mkoani Simiyu.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini akitoa ufafanuzi wa hoja, wakati wa kikao kazi kati ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (kushoto), Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma na Watumishi wa Mkoa wa Simiyu kilichofanyika katika Shule ya Msingi Bariadi Alliance mkoani Simiyu.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Simiyu (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Shule ya Msingi Bariadi Alliance mkoani Simiyu.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (kushoto) akiteta jambo na Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini wakati wa kikao kazi kati yake na Watumishi wa Mkoa wa Simiyu kilichofanyika katika Shule ya Msingi Bariadi Alliance mkoani Simiyu.
Baadhi ya Watumishi wa Umma kutoka Mkoa wa Simiyu wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Shule ya Msingi Bariadi Alliance mkoani Simiyu.
****************************
Na Happiness Shayo- SIMIYU (Bariadi)
Serikali imewataka Watendaji katika taasisi za umma kuacha vitendo
vya upendeleo wakati wa ujazaji wa fomu za OPRAS kwa watumishi
wa umma nchini ili kupima utendaji kazi wao, lengo likiwa ni kuepuka
kushusha morali ya utendaji kazi kwa watumishi hao.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa
(Mb) wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa umma mkoani
Simiyu kilichofanyika katika ukumbi wa Shule ya Msingi Bariadi
Alliance mkoani humo.
“Hakikisheni mnajaza fomu za OPRAS kiuhalisia bila upendeleo ili
kila mtumishi apate haki yake anayostahili, epukeni kuwakatisha
tamaa watumishi wanaofanya kazi kwa bidii” Dkt. Mwanjelwa
amesisitiza.
Dkt. Mwanjelwa ameweka bayana kuwa, watumishi wanaofanya kazi
pamoja wanajuana kiutendaji, hivyo si jambo zuri kwa mtendaji
kumpendelea mtumishi wakati wa ujazaji wa fomu za OPRAS.
“Serikali inahitaji OPRAS ambayo itaziba kabisa mianya ya
upendeleo”, Dkt. Mwanjelwa amehimiza.
Aidha, Dkt. Mwanjelwa amefafanua kuwa, ujazaji wa fomu za OPRAS
unatakiwa uzingatie uchapakazi wa mtumishi ikiwa ni pamoja na
tabia na mwenendo wa mtumishi kwa ujumla.
“Kuwa mtumishi wa umma ni pamoja na kuwa na mwenendo bora.
Mtumishi mwenye mwenendo mbaya hafai kuwa katika utumishi wa
umma”, Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.
Dkt. Mwanjelwa amewapongeza viongozi wa Mkoa wa Simiyu kwa
kutoa mafunzo ya OPRAS kwa watumishi wa mkoani humo na
kuwataka kuendelea kuwaelimisha watumishi ili kila mtumishi atambue haki na wajibu wake.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa kikao kazi hicho, Mkaguzi
Mkuu wa Nje wa mkoa huo, Bw. Costantine Mabirika amemshukuru
Dkt. Mary Mwanjelwa kwa kutoa elimu na maagizo ya kiutendaji,
hivyo ameahidi kuwa yatatekelezwa ipasavyo ili kuboresha utendaji
kazi wao.
Kikao kazi hicho ni muendelezo wa ziara ya Naibu Waziri, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt.
Mary Mwanjelwa (Mb) mkoani Simiyu yenye lengo la kuhimiza
uwajibikaji kwa watendaji na watumishi wa umma ikiwa ni pamoja na
kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.