Home Mchanganyiko Hospitali kuwajengea vyoo shule ya msingi Mloganzila

Hospitali kuwajengea vyoo shule ya msingi Mloganzila

0

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi
(aliyesimama) akizungumza katika mahafali ya 14 ya darasa la saba ya Shule ya
Msingi Mloganzila yaliyofanyika hii leo.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mloganzila Geofrey Magembe akielezea
jambo katika mahafali hayo.

Baadhi ya wahitimu wakiwa na walimu wao katika mahafali yaliyofanyika
shuleni hapo.

Zubeda Fadhili(kushoto) pamoja na Innocent Johanes wakisoma risala kwa
niaba ya wahitimu wa darasa la saba wa Shule ya Msingi Mloganzila.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Mloganzila Dkt. Julieth Magandi
akiwatunuku vyeti wanafunzi vya kuhitimu elimu ya msingi.

Dkt. Magandi akikata keki maalum iliyoandaliwa na uongozi wa shule kwa
ajili ya harambee ya kuchangisha fedha ya ukarabati wa majengo chakavu katika shule hiyo.

****************************

Hospitali ya Taifa Muhimbili –Mloganzila imedhamiria kujenga vyoo matundu
matano katika Shule ya Msingi Mloganzila ikiwa ni kuunga mkono juhudi
zinazofanywa na uongozi wa shule hiyo ya kuboresha mazingira ya shule ili
wanafunzi wasome katika sehemu safi na salama.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es salaam na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa
Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi alipokua akizungumza kwa niaba ya
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Lawrence Museru katika mahafali ya 14 ya
darasa la saba ya Shule ya Msingi Mloganzila.

Dkt. Magandi ameeleza kuwa ujenzi wa vyoo utagharimu shilingi milioni 10 na
kwamba utaanza mara moja ambapo vyoo vinne vitakua vya wasichana na kimoja ni kwa ajili ya watoto wenye ulemavu.

“Tulielezwa kuna hitajika matundu kumi ya vyoo hivyo kama taasisi tukaona ni
vema kusapoti suala hili ili kuhakikisha watoto wetu wanasoma katika mazingira
safi, pia tumefanikiwa kutafuta mfadhili ambaye amekubali kujenga matundu
mengine matano kwa maana hiyo matundu kumi yaliyohitajika yatakua
yamekamilika” amefafanua Dkt. Magandi.

Dkt. Magandi ametumia fursa hiyo kuikumbusha jamii kwamba jukumu la
maendeleo ya elimu ni la wananchi wote hivyo kila mmoja anapaswa kushiriki
kikamilifu.

Pia ametoa wito kwa wazazi katika kipindi hiki ambacho wanafunzi wanasubiri
matokeo ya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi waendelee kuwalea na
kuwalinda watoto ili wasijihusishe katika vitendo viovu ambavyo vitaharibu
maisha yao.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mloganzila Mwalimu
Geofrey Magembe ameishukuru Muhimbili-Mloganzila kwa msaada wa ujenzi wa
vyoo na kueleza kuwa shule hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo
ukosefu wa vyoo na uchakavu wa majengo.

Katika mahafali hayo takribani wanafunzi 100 wametunukiwa vyeti vya kuhitimu
elimu ya msingi mwaka 2019.