Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Isack Kamwelwe akiwa na wakandarasi wa kampuni ya Wu Yi wanaojenga kipande cha kilometa 108 cha Komanga Kasinde katika barabara ya Mpanda Tabora
Sehemu ya daraja la Koga linaloendlea kujengwa
……………..
Na mwandishi wetu, Katavi
Ujenzi wa daraja la Koga lenye urefu wa mita 120 linalounganisha mikoa wa Katavi na Tabora unafanyika usiku na mchana chini ya wakandarasi wa barabara wa kampuni ya kichina ya Wu Yi kwa lengo la kuhakikisha msimu wa mvua za masika unapowadia daraja hilo linapitika
Daraja hilo limekuwa likisababisha kufungwa kwa barabara ya Mpanda – Tabora kutokana na kujaa maji wakati wa mvua za masika
Akitoa taarifa kwa Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Meneja Mradi wa kampuni ya ukandarasi ya kichina ya Wu Yi bwana Li Wen Lan amesema kufikia mwezi desemba mwaka huu daraja hilo litaanza kupitika
Ameongeza kuwa tayari wameagiza vifaa vingine vya kumalizia ujenzi wa daraja hilo kutoka Afrika ya Kusini
Akiwa katika ziara ya kawaida ya kikazi mkoani Katavi Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa daraja hilo na barabara kwa ujumla
Aidha amewataka kuendelea na jitihada hizo ili kuwawezesha wakazi wa katavi kutumia daraja hilo mvua zitakapokuwa nyingi
“Koga ndio roho ya wanampanda, barabara ya Mpanda Tabora ikifungwa watu wanapata tabu sana, kwahiyo mjitahidi” alisema Kamwelwe
Naye Mkuu wa Mkoa wa Katavi bwana Juma Homera amesema maboresho yanayofanyika katika njia za reli na barabara yatainua uchumi wa mkoa kwa haraka
Pia waziri huyo amefanya ziara ya kushtukiza katika Stesheni ya Reli ya Mpanda kwa lengo la kuangalia maendeleo ya usafirishaji wa mizigo na kuzungumza na wafanyabiashara wanaotumia reli hiyo kusafirisha mizigo mbalimbali yakiwemo mazao
Wakizungumza na mheshimiwa waziri wafanyabiashara hao wametaja changamoto kadhaa wanazokabiliana nazo ukiwepo ya ubovu wa reli na ukosefu wa mahali pa kuhifadhia mazao yao
Akitoa majibu ya changamoto za wafanyabiashara waziri kamwelwe amesema serikali imekwishaanza kubadili mataruma ya reli ambapo itawezesha kubeba mzigo mkubwa na kuwa na mwendo wa kasi zaidi
Naye Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Reli Tanzania bwana Focus Sahani akitoa taarifa ya usafirishaji wa mizigo hasa mazao amesema wamekwisha safirisha mabehewa 264 na kuiingizia serikali shilingi milioni 481 kwa kipindi cha wiki mbili
Ameongeza kuwa tayari wamefanya usanifu wa kuweka jengo la kusubiria abiria na ujenzi wa maghala matatu kwa ajili ya wafanyabiashara kutunza mizigo yao wakati wanasubiria usafiri