*************************
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia Erick Mapunda kuyavunja Mabaraza yote ya Kata na Vijiji ya ardhi yasiyotenda haki wakati wa kutoa maamuzi katika wilaya ya Mafia mkoani Pwani.
Dkt Mabula alitoa agizo hilo tarehe 01 Oktoba 2019 akisikiliza kero za migogoro ya ardhi za wananchi wa Baleni na Kilindoni wakati wa ziara yake ya siku mbili wilayani Mafia mkoani Pwani kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi, kukagua masijala ya ardhi pamoja na kukagua mfumo wa ukusanyaji kodi ya ardhi kwa njia ya kielektroniki.
Alisema, kutokana na kero nyingi za ardhi alizozipokea katika ziara yake hiyo wilayani Mafia amebaini Mabaraza ya Kata na Vijiji katika wilaya hiyo hayafanyi kazi zake vizuri na wajumbe wake wamekuwa wakiyatumia kutoa maamuzi yasiyozingatia haki.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, kadri Mabaraza ya Kata na Vijiji katika wilaya ya Mafia yanavyofanya vibaya katika utoaji maamuzi yake basi hata uanzishwaji Baraza la Ardhi la Nyumba la wilaya hiyo halitafanya vizuri katika utendaji wake.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Mafia Mbaraka Dau alielezea furaha yake ya kutaka kuanzishwa Baraza la Ardhi la Nyumba la Wilaya ya Mafia ambapo alisema litasaidia kutoa haki kwa wananchi wa mafia ambao baadhi yao wamekuwa hawapati haki kutokana na kushindwa kwenda katika baraza la wilaya la Mkuranga.
Baadhi ya wananchi wa Mafia wamelalamikia Mabaraza ya Ardhi ya Kata na Vijiji katika wilaya ya Mafia pamoja na kero nyingine mbele ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa zinachangia uwepo migogoro ya ardhi.
Mohamed Shaban na Aisha Mohamed ni miongoni mwa wananchi wa Mafia waliowasilisha kero zao kwa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na hapa wanazungumza: