Home Mchanganyiko Mhandisi Malongo-Azma ya Serikali ya ujenzi wa bwawa kubwa la kufua umeme...

Mhandisi Malongo-Azma ya Serikali ya ujenzi wa bwawa kubwa la kufua umeme la Julius Nyerere iko pale pale na ujenzi wake unaendelea

0

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu Rais Mhandisi Joseph Malongo (katikati)
akizungumza wakati wa kikao na Wabunge wa Kamati ya Bunge la Ujerumani ya
Mazingira, Uhifadhi Maliasili na Usalama wa Nyuklia kilichofanyika Ukumbi wa
Ofisi ya Makamu wa Rais Jijini Dodoma. Wengine pichani kushoto ni Naibu
Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine na Mkurugenzi wa Mazingira Profesa
William Mwegoha.

Wabunge wa Kamati ya Bunge la Ujerumani ya Mazingira, Uhifadhi Maliasili na
Usalama wa Nyuklia ukiwa katika kikao na Ofisi ya Makamu wa Rais
kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi hiyo Jijini Dodoma.

Kiongozi wa Ujumbe huo Mhe. Sylvia Kotting-Uhl (katikati) akizungumza
walipokutana na Ofisi ya Makamu wa Rais Jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu Rais Mhandisi Joseph Malongo akiwa na Kiongozi
wa Wabunge wa Ujerumani Mhe. Sylvia Kotting-Uhl mara baada ya kumalizika
kwa kikao.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu Rais Mhandisi Joseph Malongo akibadilishana
mawazo na wabunge wa Kamati ya Bunge la Ujerumani ya Mazingira, Uhifadhi
Maliasili na Usalama wa Nyuklia walipowasili katika Ofisi ya Makamu wa Rais
Jijini Dodoma.

***********************************

Lulu Mussa na Robert Hokororo

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Joseph Malongo amesema
azma ya Serikali ya ujenzi wa bwawa kubwa la kufua umeme la Julius Nyerere
iko pale pale na ujenzi wake unaendelea kwa kasi huku suala la hifadhi ya
mazingira likizingatiwa.

Akizungumza na Wabunge wa Kamati ya Bunge ya Mazingira, Uhifadhi wa
Maliasili na Usalama wa Nuklia kutoka Ujerumani Mhandisi Malongo amesema
Tathmini ya Athari kwa Mazingira imefanyika na kuonyesha kuwa ujenzi huo ni
salama kwa mazingira.

“Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza mradi huu kwa kutumia fedha zake
kutoka vyanzo vya ndani. Mradi huu utachukua eneo la ukubwa wa kilomita za
mraba 1,250 ambalo ni sawa na asilimia tatu (3%) tu ya eneo lote la pori la akiba selous lenye ukubwa wa kilomita za mraba 50,000.” Malongo alisisitiza.

Mhandisi Malongo amesema kwa kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira
Na. 20 ya mwaka 2004 kifungu cha 81, mradi huu umefanyiwa tathimini ya athari kwa mazingira ili kubaini matokea hasi na chanya na kuweka mipango ya
kudhibiti madhara na kuboresha utekelelezaji wake.

Amesema kuwa kiwango cha umeme cha megawati 2,100 kitaongezeka kwenye
gridi ya Taifa kwa maendeleo ya shughuli za kiuchumi na kijamii ikiwa ni pamoja
na maendeleo ya viwanda na kupunguza uzalishaji wa gesijoto duniani, pamoja
na uwepo wa fursa za kilimo cha umwagiliaji na uvuvi ulioboreshwa katika
uwanda wa chini kutokana na usimamizi na udhibiti wa mtiririko wa maji.

Katika hatua nyingine Mhandisi Malongo amewafafanulia wabunge hao
mafanikio yaliyopatikana katika katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki hapa
nchini lililoanza kutekelezwa Juni Mosi na kusema kuwa katika kipindi cha miezi
mitatu kampeni hiyo imeonyesha mafanikio kwa kiasi kikubwa kwani
imepokelewa kwa mtazamo chanya na wanachi ikiwa ni jitihada za kushirikisha
taasisi mbalimbali na wadau kwa ujumla.

Akiongea kwa niaba ya wenzake kiongozi wa ujumbe huo Mhe. Sylvia Kotting-
Uhl ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa mageuzi makubwa yanayofanyika
katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano na kuahidi ushirikiano na nchi yake
katika kujenga uwezo katika nyanja za kusimamia na kudhibiti taka za
kielektroniki, Uzalishaji wa Umeme wa jua na kutoa mwaliko kwa ujumbe wa
Tanzania kutembelea Ujerumani kujifunza zaidi.