Mkurugenzi wa Utafiti,Mafunzo na Ugani kutoka wizara ya mifugo Dkt.Angello Mwillawa,akifafanua jambo kwa washiriki sehemu ya pili ya mafunzo rejea kwa wataalam wa malisho kutoka mashmba ya serikali na wadau wa malisho nchini wakati akifundishi mada mbalimbali zinazohusiana na malisho kushoto kwake ni Afisa mifugo Mkuu Idara ya malisho na Rasilimali ya vyakula vya mifugo Israel Kilonzo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika chuo cha Mifugo Lita Mpwapwa.
Mkurugenzi wa Utafiti,Mafunzo na Ugani kutoka wizara ya mifugo Dkt.Angello Mwillawa,akifundisha mada mbalimbali kwa washiriki sehemu ya pili ya mafunzo rejea kwa wataalam wa malisho kutoka mashmba ya serikali na wadau wa malisho nchini yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika chuo cha Mifugo Lita Mpwapwa.
Mkurugenzi wa Utafiti,Mafunzo na Ugani kutoka wizara ya Mifugo Dkt.Angello Mwillawa,akiwaonyesha washiriki wa semina ya mafunzo rejea kwa wataalam wa malisho kutoka mashamba ya serikali na wadau wa malisho nchini walipotembelea shamba la malisho TALIRI lililopo Vianze yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika chuo cha Mifugo Lita Mpwapwa.
………………….
Na Alex Sonna, Mpwapwa
MAFUNZO rejea kwa wadau na wataalam wa malisho kutoka mashamba ya serikali nchini, yamehitimishwa ,huku Wizara ya Mifugo ikisisitiza uzalishaji wa mashamba ya malisho bora.
Mafunzo haya ya siku mbili yamefanyika katika Chuo cha LITA kampasi ya Mpwapwa mkoani Dodoma.
Akizungumza baada ya kuhitimisha mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara hiyo, Dk.Angello Mwillawa, amesema lengo la uzalishaji huo ni kuwa na malisho yanayozaa kwa wingi na yana ubora unaomsaidia mnyama kupata virutubisho sahihi.
“Wizara imeona umuhimu wa jambo hili kwa kushirikiana na taasisi zake imewaleta pamoja watendaji na wataalam katika mafunzo hayo ili kuwa na mikakati ya kuzalisha malisho bora,”amesema.
Aidha, amesema kumekuwepo na mikakati mbalimbali ya wizara ikiwa ni pamoja na udhibiti wa magonjwa ya mifugo na matumizi ya madawa na viuatilifu kuhakikisha mifugo ipo katika ubora unaotakiwa.
Amesema Wizara imekuwa ikitekeleza mkakati wa upatikanaji wa malisho na maji kwa nchi nzima, jambo ambalo limekuwa likitiliwa mkazo na Wizara hiyo namna bora ya kuhakikisha nyanda za malisho na maeneo ya machunga yanaboreshwa ili kujitosheleza na malisho mwaka mzima.
“Tumekuwa tukihakikisha zile nyanda zetu za malisho wafugaji wanapata elimu ya kutosha na watumiaji wengine wa nyanda za malisho kwa kuhakikisha kunakuwa na matunzo na matumizi endelevu ya malisho,”amesema.
Naye, Afisa Mifugo Mkuu Idara ya malisho na rasilimali ya vyakula vya mifugo kutoka wizara hiyo, Israel Kilonzo, ameongeza kusema kuwa mafunzo hayo ni kuwa na uelewa wa pamoja katika uzalishaji wa malisho na kutunza nyanda za malisho.
“Wazingatie yale waliyofundishwa waende kufanya kazi ili kufikia malengo ambayo wamejiwekea katika kuhakikisha tunazalisha malisho ya kutosha,”amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa kampas ya LITA Mpwapwa, Moses Mlahagwa, amesema ili mifugo izalishe maziwa na nyama ya kutosha lazima wapate chakula cha kutosha.
“Hii imekuwa ni changamoto katika uzalishaji mazao ya mifugo yamekuwa ni hafifu kwasababu hakuna lishe ya kutosha, hapa kwenye mafunzo tumeona changamoto hizi sasa tunaweza kuchukulia kama fursa ya kupiga hatua kwenye uzalishaji,”amesema
Hata hivyo, amesema chuo hicho kipo kwenye mpango kuwa na maeneo makubwa ya uzalishaji malisho hivyo ni fursa nzuri kwao kuhakikisha wanaingia kwenye eneo la uzalishaji kwa kupata uzoefu wa kutosha kutoka kwa wadau wengine.
Kadhalika, Meneja masoko kutoka Ranchi za Taifa(Narco), Mzava Emmanuel, amesema kuna wakati nchi iliwahi kukumbwa na ukame na mifugo kufa haipaswi kujirudia tena kwa kuwa wataalam wapo.
“Tufike sehemu kama taifa tuwe na ghala la malisho hata itakapotokea njaa ya malisho kwa miaka miwili kusiwe na mifugo inayokufa bali walishwe kupitia hifadhi ya malisho itakayokuwepo,”amesema.
Nao baadhi ya washiriki, Wameshukuru Wizara kwa kuwapatia mafunzo hayo yatakayosaidia kupiga hatua katika kuhakikisha kunakuwepo na malisho ya kutosha kwa ajili ya mifugo.
Afisa Mifugo kutoka shamba la mifugo Mabuki na mtaalam wa malisho, Asteria Mwaya amesema ili kuwa na mbegu bora ya malisho kunapaswa shamba liandaliwe vyema, kuvunwa na kuhifadhiwa vizuri.
“Tumepata ujuzi ambao unatusaidia kufanya kazi eneo lolote hata kama una rasilimali chache unaweza kufanya vizuri na kwa tija, na kusaidia kutoa elimu kwa wananchi kuondokana na uingizaji ng’ombe kwenye shamba la serikali na kujitengenezea malisho yao wenyewe,”amesema.