Home Mchanganyiko WAZIRI JAFO-VITENDO VYA WIZI WA MITIHANI VIKEMEWE

WAZIRI JAFO-VITENDO VYA WIZI WA MITIHANI VIKEMEWE

0

Na.Alex Sonna,Dodoma

Imeelezwa kuwa vitendo vya wizi wa mitihani ni fedheha na ni jambo linalo poromosha elimu ya Tanzania na wito umetolewa  kwa walimu kutojihusisha na vitendo kama hivyo kulinda elimu yetu.

Hayo yamesemwa  jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,(TAMISEMI) Selemani Jafo, wakati  alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa kwanza wa wenyeviti wa walimu wakuu wa shule za msingi Tanzania bara.

Waziri Jafo amesema wizi wa mitihani sio sifa nzuri na njema kwa taifa letu hivyo amewataka walimu wahakikishe wanasimamia kanuni na weledi kwenye masuala ya mitihani, amesema angalau kwa Sasa vimepungua.

“Nidhamu katika usimamizi wa mitihani kwa sasa imerudi nikupongeze sana Msonde kwa hili, ukifanya wizi wa mitihani jambo hili lina gharama kubwa kwa taifa, niwasihi nyinyi mliopewa dhamana katika  hili,nendeni mkafanye compliers (utekelezaji) suala zima kwa kuzingatia kanuni na kusimamia weledi.” amesema Waziri Jafo.

Amebainisha kuwa mwaka huu Ofisi yake itatoa tuzo ya ufanyaji vizuri wa mitihani ili kuleta motisha kwa walimu wetu kufanya vizuri katika kusimamia mitihani.

Pia amesema uimarishaji wa miundombinu umekuwa ni mkubwa ambapo lengo la Rais ni kuhakikisha watoto wote wanapata fursa ya elimu na kusoma katika mazingira mazuri.

“Pamoja na fedha zinazotolewa kwa ajili ya elimu bila malipo, pia serikali imetoa zaidi ya Sh.Bilioni 305.1 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ikiwemo ujenzi wa nyumba za walimu, madarasa, matundu vya vyoo, maabara na maboma” amesema Jafo.

Ameongeza kuwa “Ajenda ya elimu kwa sasa inaenda kwa kasi sana, bajeti ya mwaka huu tumetenga sh bilioni 288.247, katika program ya elimu bila malipo na kutoa zaidi ya Sh bilioni 24 kila mwezi, ikiwamo sh bilioni 3.2 ambazo ni kwa ajili ya posho za walimu” amesema.

Kuhusu maboresho ya shule kongwe, Jafo amesema walibainisha shule kongwe 89 ambazo zilikuwa katika hali mbaya na kuwa mpaka sasa shule 43 tayari zimekabilika kufanyiwa maboresho huku zilizobaki zikiwa katika hatua mbalimbali ya kuboreshwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa walimu wakuu wa shule za msingi Tanzania bara,  Rehema Ramole, amesema walimu hao wanasikitishwa na walimu wenzao wanaojihusisha na udanganyifu kwenye mitihani ya darasa la saba.

Pia ameongeza “Tunapongeza serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli kwa kuipa kipaumbele sekta ya elimu, tutaendelea kushikamana nae bega kwa bega kuhakikisha tunatekeleza yale yaliyoahidiwa kwenye ilani ya uchaguzi,”amesema Rehema