Home Mchanganyiko Serikali Kutumia Bilioni 100 Kumaliza Tatizo la Maji Kilwa

Serikali Kutumia Bilioni 100 Kumaliza Tatizo la Maji Kilwa

0

Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa akipokea taarifa ya ujenzi wa tenki la maji la Mradi wa Maji wa Mpigamiti uliopo katika Wilaya ya Liwale, mkoani Lindi. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Sarah Chiwamba.

Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa akikagua ujenzi wa tenki la maji la Mradi wa Maji wa Mpigamiti uliopo katika Wilaya ya Liwale, mkoani Lindi.

Tenki la maji la Mradi wa Maji wa Mpigamiti katika Wilaya ya Liwale, mkoani Lindi.

Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa akisalimiana na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa mara baada ya kuwasili wilayani hapo, kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai.

Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) akiwa na baadhi ya viongozi wa Wilaya ya Kilwa, wa pili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai.

Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) akihutubia wakazi wa Kilwa Kivinje katika Wilaya ya KIlwa, mkoani Lindi.

………………….

Serikali imepanga kutumia Shilingi bilioni 100 katika kufanikisha utekelezaji wa mkakati wa kumaliza tatizo la maji la muda mrefu katika mji mkongwe wa Kilwa, mkoani Lindi. 

Mpango huo ni wa muda mrefu wa kufikisha huduma ya majisafi na salama kwa wananchi wa Kilwa, ni sehemu ya utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya maji katika miji 29 nchini Kilwa ikiwa ni mji mmojawapo, utakaogharimu jumla ya Shilingi trilioni 1.2 zinazotokana na mkopo wa bei nafuu kutoka Benki ya Exim ya India.

Akitoa ufafanuzi wa utekelezaji wa mradi huo mbele ya wakazi wa Kilwa Kivinje, Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa amesema kazi ya upembuzi yakinifu imeshakamalika na taarifa zake zipo nchini India kwa ajili ya kupata kibali, akisema baada ya kupata kibali Serikali itatangaza zabuni na ifikapo Januari, 2020 inatarajia kumpata mkandarasi na kuanza kazi.

Profesa Mbarawa amesema jumla ya gharama za ujenzi wa mradi huo ni Shilingi bilioni 100 na utamaliza kabisa tatizo la maji Kilwa. Lakini akisema kuwa kabla ya mradi huo kuanza, utekelezaji wa mradi wa maji wa Shilingi bilioni 1.3 utakaohudumia maeneo ya Kilwa Kivinje, Kipatimu, Somanga na Pande utaanza hivi karibuni kama mpango wa muda mfupi wakati wakisubiri mradi huo mkubwa.

‘‘Niwatoe hofu wananchi wa Kilwa kuwa tutaanza kutekeleza mradi wa maji kama suluhisho la muda mfupi, wakati utaratibu wa ujenzi wa mradi mkubwa ukiendelea. Tutatoa kipaumbele kwa maeneo yenye changamoto kubwa ya maji ikiwemo kwa kuwa ndio lengo la Serikali’’, Profesa Mbarawa amesema.

Akitoa shukrani zake kwa Serikali kwa niaba ya wakazi wa Kilwa, Mbunge wa Jimbo la Kilwa, Salum Bungala amesema hakika wamefarijika sana na jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kumaliza tatizo la maji mjini Kilwa na inathibitisha kwa vitendo kuwa maendeleo hayabagui itikadi za kisiasa kwa kupeleka maendeleo kwa wananchi wote.

Awali, Waziri wa Maji, Profesa Mbarawa alikagua Mradi wa Maji wa Mpigamiti uliopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Liwale na kubaini mapungufu katika ujenzi wa tenki la maji la huo yanayosababisha usalama wa tenki hilo kuwa mdogo.

Akitoa maelekezo baada ya kukuta mapungufu hayo, Profesa Mbarawa amesema ataunda timu ya wataalam kwa ajili ya kuchunguza, kubaini tatizo na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa. Akisisitiza kuwa endapo uwezekano wa kukarabati tenki hilo utashindikana, itabidi lijengwe tenki jipya.

Hata hivyo, ametoa onyo kwa Kampuni ya Don Consult ambayo ilifanya kazi ya usanifu wa mradi huo akisema kuwa endapo itabainika mapungufu hayo yametokana na uzembe wao ni lazima achukue hatua stahiki kwa kampuni hiyo.

Akisisitiza Serikali haitarudia tena makosa ya kuwekeza fedha nyingi bila kupata matokeo chanya kwenye miradi ya maji na kila mradi utakaokamilika ni lazima uwe na thamani halisi ya fedha zilizotumika.

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa amemaliza ziara yake mkoani Lindi kwa kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya maji katika wilaya zake zote za Lindi, Ruangwa Nachingwea, Liwale na Kilwa.