************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) afuatilie sababu za mikoa ya Tanga na Njombe kutotekeleza sheria ya kutoza asilimia tano ya ushuru unaotokana na mazao ya misitu.
Amesema makampuni yanayonunua nguzo lazima yahakikishe yanazingatia sheria ya nchi ikiwemo ulipaji wa kodi zilizowekwa kwa mujibu wa sheria na kampuni zote zilizonunua nguzo bila ya kulipa kodi zifuatiliwe na zilipe kodi yote waliyoikwepa.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Septemba 26, 2019) wakati alipotembelea kiwanda cha kutengeneza nguzo za umeme cha Qwihaya kilichoko Mafinga wilayani Mufindi akiwa katika siku ya tatu za ziara yake ya kikazi mkoani Iringa.
“Naibu Waziri TAMISEMI hakikisha unakwenda mkoani Njombe na uaanze kuzungumza na mkuu wa mkoa, tunataka kujua kwa nini hawajaanza kutekeleza sheria ya kutoza asilimia tano ya ushuru unaotokana na mazao ya misitu hali iliyosababisha wanunuzi kumbilia huko na kuacha kununua mazao hao katika mkoa wa Iringa.”
“Tunataka tujue ni nani huyo anayewakataza wasilipe kodi na tuangalie anamahusiano gani na viongozi wa mkoa huo. Ukaangalie makampuni hayo yanamahusiano gani na viongozi hao hadi wasilipe kodi na tutajua kama kampuni hizi ni zao au za ndugu zao.”
Waziri Mkuu amesema Serikali itahakikisha inawabana wafanyabiashara wote walionunua nguzo kwenye mikoa hiyo ambao hajalipa asilimia tano ya ushuru unaotokana na mazao ya misitu ili waweze kulipa kiasi chote walichokikwepa..
Amesema Serikali inahitaji kodi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na haoni sababu ya mikoa hiyo kushindwa kutoza kodi iliyowekwa kwa mujibu wa sheria. Kitendo cha mikoa hiyo kutotoza kodi hakikubaliki na wafanyabiashara wote waliochukua nguzo bila ya kulipa kodi hiyo watalipa kodi yote kuanzia walipioanza kuchukua nguzo.
Waziri Mkuu amesema Serikali imeweka mikakati ya wafanyabiashara wafanye biashara zao katika mazingira bora na kwa kuzingatia sheria za nchi na pia Rais Dkt. John Magufuli amezuia nguzo zote za umeme kuagizwa kutoka nje ili kuwawezesha wafanuyabiashara wa ndani kuuza nguzo pamoja na wananchi kupata ajira.
“Hata tulipokuwa tunanunua nguzo kutoka nje zilikuwa zinatoka hukuhuku na walichokuwa wakifanya ni kuzichukua huku na kuzipeleka nchi jirani na kuziweka kwa wiki kisha wanabadilisha vibao na kuzirudisha tena nchini.”
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Happi alimweleza Waziri Mkuu kwamba wateja wa mazao ya misiti wameanza kupungua na kwenda mikoa ya Tanga na Njombe kwa kuwa katika mikoa hiyo haijaanza kutekeleza sheria ya kutoza asilimia tano ya ushuru unaotokana na mazao ya misitu, hivyo ameiomba Serikali iwasaidie.
Kwa upande wake, Meneja wa Kiwanda cha kutengeneza nguzo za umeme cha Qwihaya, Benedicto Mahenda alisema kiwanda hicho kilianzishwa 2007 kwa ajili ya uchakataji wa mbao na 2016 kilianza kuzalisha nguzo za umeme wakiwa na mtambo wenye kuzalisha nguzo 100 kwa siku. Kiwanda kimeajiri watumishi 350.
Meneja huyo alisema katika kuitikia wito wa Rais Dkt. Magufuli wa kujenga uchumi kupitia sekta ya viwanda, walifanya mabadiliko kwa kujenga kiwanda kikubwa na cha kisasa cha kuzalisha nguzo za umeme chenye uwezo wa kuzalisha nguzo 1,500 kwa siku.
Alisema malighafi za kiwanda hicho wanazipata kutoka katika shamba la miti la Sao Hill lililoko chini ya Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) na kwenye mashamba ya wakulima wadogo. Soko kubwa la bidhaa zao ni TANESCO kupitia utekelezaji wa miradi ya REA.
Pia, Meneja huyo alimshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa uamuzi wake wa kuzuia nguzo zisitoke tena nje ya nchi na kutumia nguzo zinazozalishwa na viwanda vya ndani. “Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutuamini na kututia moyo wawekezaji wa ndani na kutuonyesha soko la kuuza bidhaa zetu.”