Home Mchanganyiko UHABA WA MAJI WAWALIZA WANANCHI WILAYANI IKUNGI MKOANI SINGIDA

UHABA WA MAJI WAWALIZA WANANCHI WILAYANI IKUNGI MKOANI SINGIDA

0

 Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo akimtwika ndoo ya maji mwanafunzi wa Sekondari ya Mwaru, Zafarani Selemani baada ya kukagua mradi wa maji shuleni hapo mwishoni mwa wiki.
 DC Mpogolo akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mwaru.
 DC Mpogolo akiwa na viongozi wa Kata ya Mwaru baada ya kukagua jengo la maabara katika Shule ya Sekondari ya Mwaru.
 DC Mpogolo akizungumza na viongozi baada ya kukagua ujenzi wa madarasa mawili na ofisi ya walimu katika  Shule ya Msingi Mtakuja.
 Mkutano wa ndani ukiendelea.
 Afisa Tarafa ya Sepuka Cornel Nyoni akiwatambulisha viongozi mbalimbali mbele ya DC Mpogolo kabla ya kuanza kwa mkutano wa ndani.
 DC Mpogolo akizungumza na viongozi wa Kata ya Mwaru katika mkutano wa ndani. Kutoka kushoto ni Diwani wa Viti Maalumu wa Tarafa ya Sepuka, Theresia Masinjisa, Diwani wa Viti Maalumu wa Kata ya Sepuka, Halima Athumani Ng’ura na Diwani wa Kata ya Mwaru, Iddi Makangale.
 Hapa DC Mpogolo akizungumza na viongozi baada ya kukagua ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Mlandala.
 Wananchi na wanafunzi wakisubiri kuteka maji kwenye bomba la Kijiji cha Mlandala.
 Wakazi wa Kijiji cha Mlandala, Moshi Mohamed (kulia) na Salma Athumani wakitoka kuteka maji katika bomba la Kijiji cha Mlandala.
 Mkazi wa Kijiji cha Mlandala, Ramadhani Kamata akizungumzia changamoto ya maji katika kijiji hicho.
DC Mpogolo akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Kata ya Mwaru baada ya kumaliza ziara ya kukagua miradi 
 
 
Na Dotto Mwaibale, Singida
 
KUKOSEKANA kwa  maji ya uhakika katika Kijiji cha Mlandala Wilayani Ikungi mkoani Singida baada ya tenki kupasuka kumesababisha wananchi kuwa na changamoto ya maendeleo.
 
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya Mkuu wa Wilaya  Edward Mpogolo mwishoni mwa wiki alipokuwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi katika kata za Sepuka, Mwaru na Irisya pamoja na kujitambusha baada ya kuteuliwa kuongoza wilaya hiyo waliiomba serikali kuwasaidia kuondoa changamoto hiyo.
 
Walisema wanatumia muda mwingi kusubiria kupata maji na kushindwa kufanya shughuli zingine za maendele.
 
” Hapa kijijini kwetu mwaka 2016 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi  ilituletea mradi wa maji lakini unaendeshwa kwa hasara kwani maji yote yanaishia njiani baada ya tenki kupasuka ” alisema Ramadhani Kamata.
 
Kamata alisema mbali ya hasara hiyo ya kumwagika maji changamoto nyingine ni matumizi ya jenereta kwa ajili ya kusukuma maji kwenda kwenye tenki ambapo kila siku wanatumia lita mbili za dizeli ambazo ni sh.5000.
 
Kamata aliongeza kuwa awali halmashauri hiyo iliwaambia itawanunulia betri litakalo kuwa likisukuma jenereta hilo lakini hadi leo hii hawajapata.
 
 Salma Athumani alisema kupasuka kwa tenki hilo kunasababisha wananchi kutumia muda mrefu kusubiri maji katika bomba hilo moja linalo hudumia wananchi wa kijiji hicho.
 
Alisema katika bomba hilo kila ndoo moja wanachangia sh.50 hela aliyodai ni nyingi kwa wananchi kutokana na matumizi makubwa ya maji.
 
” Kutokana na maji kutoka kidogo wanafunzi wa shule yetu ya msingi ya Mlandala wanalazimika kutembea umbali wa kilometa mbili kuchota maji ya kisima kwa ajili ya matumizi ya shuleni” alisema Moshi Mohamed.
 
Mohamed alisema muda huo wanao tumia wanafunzi hao kwenda kuchota maji unaweza kuwaathiri katika masomo yao na kujikuta wakishuka kitaaluma.
 
Aliongeza kuwa foleni ya kusubiri maji ikiwa kubwa wanalazimika kwenda kutafuta maji ya visima katika vitongoji vya Idodoma na Uzelela ambavyo vipo nje kidogo ya Kijiji cha Mlandala.
Mkuu wa wilaya  Edward Mpogolo baada ya kusikia changamoto hiyo aliahidi kuonana na mhandisi wa ujenzi wa wilaya ili kufika katika kijiji hicho kwa ajili ya kulifanyia ukarabati tenki hilo au kununua tenki kubwa la plastiki litakalotumika kwa muda ili kupunguza makali ya changamoto hiyo.
 
Aliongeza kuwa Serikali imekwisha toa sh. 1.5 bilioni kwa ajili ya uchimbaji wa visima 28 na sh. 2 bilioni kwa ajili ya usambazaji wa maji na ujenzi wa matenki kwa majimbo yote mawili ya Singida Mashariki na Magharibi na pindi mradi huo utakapo kamilika utamaliza kabisa changamoto ya maji katika wilaya hiyo.