Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe kulia akimkabidhi Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Profesa Iddris Mshoro nyaraka za kufanyia kazi zilizoandaliwa na Wakala huo mara baada ya kuzindua rasmi Bodi ya Ushauri (MAB) katika kikao kilichofanyika katika ofisi za TEMESA Keko jijini Dar es Salaam jana.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle kulia akizungumza wakati akimkaribisha Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe kuzindua rasmi Bodi ya Ushauri ya Wakala huo katika kikao kilichofanyika katika ofisi za TEMESA Keko jijini Dar es Salaam jana.Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe akisisitiza jambo wakati akizungumza na wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) pamoja na viongozi waandamizi wa Wakala huo (hawapo pichani) wakati wa kikao cha uzinduzi wa bodi hiyo kilichofanyika katika ofisi za TEMESA Keko jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Mtendaji Mkuu wa TEMESA Mhandisi Japhet Y. Maselle.
Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe akiwa katika picha ya pamoja na Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) mara baada ya kuizindua rasmi jana. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo Profesa Iddris Mshoro na kulia kwake ni Mtendaji Mkuu wa TEMESA Mhandisi Japhet Y. Maselle.
PICHA ZOTE NA ALFRED MGWENO (TEMESA).
**************************
NA ALFRED MGWENO- TEMESA DAR ES SALAAM
Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Katibu Mkuu na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kupitia Mtendaji Mkuu wamesaini mkataba wa utendaji kazi wa Wakala huo ambapo ndani yake ipo miradi yenye thamani ya shilingi Bilioni 66.5 itakayotekelezwa na TEMESA katika mwaka huu
wa fedha 2019/2020.
Hayo yamebainishwa jana na Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Mh. Mhandisi Isack Kamwelwe alipokuwa akizungumza wakati akizindua rasmi bodi ya Ushauri ya Wakala huo jijini Dar es Salaam itakayoongozwa na Mwenyekiti wake Profesa Mhandisi Idriss Mshoro. Mhandisi Kamwelwe amesema
kati ya fedha hizo, Wizara imetoa kiasi cha shilingi bilioni 22.6 ili kusaidia mchakato huo.
‘’Hivi karibuni mtaona jinsi serikali ilivyochukua hatua na juhudi za makusudi kuiboresha TEMESA kwa kuongeza bajeti ya Wizara ya Huduma za Ufundi kutoka shilingi bilioni 17.5 hadi kufikia shilingi bilioni 53.1 ni jukumu la bodi kuhakikisha inasimamia kwa karibu matumizi ya fedha hizo baada ya serikali
kufanya juhudi zote.’’ Alisema Mhandisi Kamwelwe.
Waziri Kamwelwe Aliongeza kuwa Wizara mpaka hivi sasa tayari imekwishatoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 12.5 kwa ajili ya kutekeleza maboresho hayo.
Kuhusu madeni ambayo TEMESA inazidai Taasisi za Umma na Wizara, Mhandisi Kamwelwe alisema Wizara imekwishawasilisha barua Wizara ya Fedha na Mipango ya kuomba deni la shilingi bilioni 19.7 lilipwe mara moja na Hazina ambapo alisisitiza hatua hiyo itasaidia siyo tu kujiimarisha bali pia kulipa
madeni ya Wazabuni wanaoidai.
Awali Mtendaji Mkuu wa Wakala huo Mhandisi Japhet Maselle, akifungua kikao hicho alimshukuru Waziri Kamwelwe kwa kuteua bodi hiyo na kuahidi kutoa ushirikiano wa karibu ili kufanikisha malengo.
‘’Naomba nikushukuru kwa uteuzi wa Bodi ya Wakala na uamuzi wako wa kuizindua leo ili iweze kuanza kazi rasmi, aidha nikuombe utakapokuwa umemaliza uzinduzi wa bodi, uwakabidhi wajumbe wa bodi nyaraka muhimu za kufanyia kazi ambazo zimeandaliwa na Wakala kufuatia maelekezo yako katika
barua yako wakati wa uteuzi wao,’’ aliongeza Mhandisi Maselle.
Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo Profesa Mhandisi Idriss Mshoro alimshukuru Waziri Kamwelwe kwa kuwaamini yeye na wajumbe wenzake kuitumikia bodi ya Wakala huo ambapo aliongeza ni jukumu kubwa wamepewa na kuahidi kutimiza majukumu hayo na matarajio ya serikali na wizara kwa ujumla.
Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) inaundwa na wajumbe Cunbert Kapilima kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mhandisi Boniface Kulaya kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Dkt Benjamin Ndimila kutoka Chuo cha Usafirishaji (NIT), Mhandisi Deogratias
Nyanda kutoka Shirika la Nyumbu (TACT) pamoja na Sunday Hyera kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Bodi hiyo imeanza rasmi utekelezaji wa majukumu yake.