Home Mchanganyiko MIKAKATI YA SERIKALI KUFUFUA ZAO LA KOROSHO KUREJESHA FURAHA YA WAKULIMA

MIKAKATI YA SERIKALI KUFUFUA ZAO LA KOROSHO KUREJESHA FURAHA YA WAKULIMA

0

 

Na Ismail Ngayonga,MAELEZO

DAR ES SALAAM

SEKTA ya Kilimo nchini imeendelea   kuwa   ni   Sekta   muhimu   katika maendeleo ya uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla hususan katika wakati huu tunapojizatiti kufikia uchumi wa viwanda.

Katika mwaka 2017, sekta hiyo ilitoa ajira kwa Watanzania kwa asilimia 65.5, ikichangia asilimia 28.7 ya Pato la Taifa ambapo sekta ndogo ya mazao ilichangia asilimia 16.58.

Takwimu zinaonesha kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka 2018, ukuaji wa Sekta ya Kilimo ulifikia asilimia 7.1, ukuaji huo ulichangiwa na hali nzuri ya hewa na jitihada za Serikali za kuhakikisha kuwa pembejeo zinawafikia wakulima kwa wakati.

Kutokana na matumizi yasiyoridhisha ya pembejeo muhimu na kutozingatiwa kwa kanuni bora za kilimo, Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa kuwezesha pembejeo muhimu zikiwemo mbegu bora, mbolea na viuatilifu kuwafikia wakulima kwa wakati.

Takwimu zinaonesha kwamba matumizi ya zana bora za kilimo yanaongezeka miongoni mwa wakulima ambapo kwa mwaka 2018 wastani wa kitaifa wa matumizi ya zana bora za kilimo umeongezeka hadi kufikia asilimia 20 kwa matrekta na asilimia 27 kwa wanyama kazi ikilinganishwa na asilimia 14 ya matrekta na asilimia 24 ya wanyama kazi mwaka 2013.

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeendelea kuimarisha mifumo ya masoko na kuratibu mazao makuu ya kimkakati ikiwemo korosho, tumbaku, kahawa, chai na pamba hatua iliyosaidia  kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao hayo kutoka tani 901,641 mwaka 2016/2017 hadi tani 967,184 mwaka 2017/2018.

Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2019/2020, Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga anasema katika msimu wa 2018/2019, Wizara ya Kilimo ililenga kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara hadi kufikia tani 1,356,368 ambapo hadi kufikia mwezi Machi 2019, takribani tani 667,631 ikiwa ni sawa na asilimia 49.2 ya lengo zimezalishwa.

Kuhusu zao la korosho, Waziri Hasunga anasema katika kuendeleza zao hilo Serikali imesambaza miche bora 12,252,197 katika mikoa 17 inayolima zao hilo kati ya miche 13,661,433 iliyozalishwa kupitia mikataba iliyoingiwa msimu wa 2017/2018 baina ya Bodi ya Korosho na wazalishaji 678.

Hasunga anasema katika mwaka 2018/2019, mbegu za korosho kilo 47,484 ambazo zitazalisha miche 6,647,760 ya kutosheleza ekari 391,045 zimezalishwa na Kituo cha Utafiti cha Naliendele na kusambazwa katika mikoa 20 na uzalishaji wa miche unaendelea.

“Mwaka 2018/2019, Wizara imesimamia ununuzi wa pembejeo za zao la korosho kwa utaratibu wa pamoja kupitia zabuni na Vyama vya Ushirika ili kuhakikisha kuwa wakulima wanapata pembejeo kwa wakati na kwa bei nafuu” anasema Waziri Hasunga.

Anaongeza kuwa kupitia utaratibu huo, jumla ya tani 31,500 na lita 520,000 za salfa zimenunuliwa ambapo wakulima wamenunua jumla ya tani 1,994.175 na lita 14,283 na bakaa ya viuatilifu vilivyonunuliwa kwa njia ya zabuni ni tani 29,505.825 na lita 505,717 za salfa ambavyo vinaendelea kuuzwa kwa wakulima kwa ajili ya msimu wa 2019/2020.

Akifafanuza zaidi Waziri Hasunga anasema Wizara kupitia Bodi ya Korosho inaendelea na usajili wa wakulima wa korosho ambapo hadi kufika Machi 2019, wakulima 200,000 wamesajiliwa, ambapo bodi hiyo pia  imeandaa mfumo endelevu ambao utawawezesha maafisa katika kila Halmashauri kukusanya na kuhuisha taarifa kwa kutumia simu za mkononi.

Katika upande wa mafunzo, Hasunga anasema Serikali imeendesha mafunzo ya udhibiti ubora wa korosho ghafi kwa wataalamu 63 katika Halmashauri za Mkuranga, Kibiti, Masasi, Ruangwa, Nachingwea na Tunduru na kuhusisha wataalamu kutoka Bodi ya Usimamizi ya Stakabadhi za Ghala, waendesha ghala na wanunuzi.

Hadi kufikia tarehe 30 Aprili 2019, jumla ya tani 222,825 zimekusanywa kutoka kwa wakulima, kati ya hizo tani 211,184 zimehakikiwa na tani 177,357 zenye thamani ya Tsh Bilioni 578.5 zimelipwa kwa wakulima 379,283, na hizo kuuzwa korosho kwa bei elekezi  ya Tsh 3,300 kwa kilo ya korosho ghafi daraja la kwanza na Tsh. 2,640 kwa kilo ya korosho ghafi daraja la pili bila makato.