Home Michezo TUSIPOJUA TATIZO LETU, HATUWEZI KUJIKWAMUA

TUSIPOJUA TATIZO LETU, HATUWEZI KUJIKWAMUA

0

Na.Imani Kelvin Mbaga,Dar es Salaam
Ni siku nyingine tena katika ulimwengu wa soka tukiwa tumegubikwa na giza la manung’uniko lukuki baada ya matokeo ya karaha yaliyotanguliwa na hamasa.
Kila mtu anasema lake, wapenda mpira hawataki kusikia la muazini wala mnadi Swala hali ni tafrani.
Mbaya zaidi tunatafuta mchawi tusiyemjua, wala aina ya uchawi aliyotumia, hatuna mwaguzi wala mwombezi atakayetutoa tulipo kwakuwa tumefunga macho ya ufahamu kuona ukweli, tunaamua kubahatisha hivyo tutegemee kudra.
Tatizo siyo Ndayiragije, Maganga, Chilunda wala Mkude, kwa nn mnamuacha Karia na kamati nzima utendaji kwa maana ya TFF?
Huwezi kufika popote kama huna mipango,mikakati na utashi katika maisha yako.
Hivi kuna mtu anajua dira yetu katika michezo Tanzania?
Wana siasa wana mpango wa taifa je? Wana soka wana nn?
Hivi lengo letu sisi ni lipi na kwa muda gani? Tunataka kwenda CHAN. AFCON au WORLD CUP?
Huyu Ndayiragije mmempa lengo gani na kwa muda gani ili mumdai?
Nahodha wa timu yetu ya taifa amesema kama kuna kitu anatamani basi ingekuwa ni kucheza ulaya mapema kuliko sasa angalau akiwa na miaka 18, sijuwi kama alieleweka kwa kusema hivyo. Chukua sentensi yake hiyo kisha anza kuwaza kuhusu Serengeti boys na Ngorongoro heroes utaelewa tu.
Mwisho nifikishieni ujumbe wangu kwa wadau wa soka, tuache kuwapigia kelele na kuwatukana wachezaji wetu na tuwageukie waliohodhi mpira wetu huku wakisubiri ruzuku, faini na viingilio ili wakamilishe mipango ya familia zao
Kwa heri kwa sasa