Mbunge wa Jimbo la Kwimba Mhe. Shanif Mansoor (CCM) (katikati) akinawa mikono wakati wa sherehe za kupokea mradi wa maji wa Kijiji cha Shilima, Kata ya Kikubiji, Wilaya ya Kwimba, Mkoani Mwanza. Kulia ni Diwani wa Kata ya Kikubiji, Alfred Luteja.
Mbunge wa Jimbo la Kwimba Mhe. Shanif Mansoor (CCM) (katikati) akinywa maji ya Mradi wa Kijiji cha Shilima wakati wa sherehe za kupokea mradi huo.
Wananchi wa Shilima wakijipatia huduma ya maji kutoka kwenye mradi uliyozinduliwa hivi karibuni ambao unatoa maji kutoka Ziwa Victoria.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Shilima na vijiji vya jirani wakimsikiliza Mbunge wao Shanif Mansoor (hayupo pichani) wakati wa sherehe za kuupokea mradi wa maji wa Shilima.
***********************
Mbunge wa Jimbo la Kwimba Mhe. Shanif Mansoor (CCM) ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa kukamilisha mradi wa maji wa Kijiji cha Shilima, Kata ya Kikubiji Wilaya ya Kwimba, Mkoani Mwanza.
Ametoa pongezi hizo jana alipojumuika na wapiga kura wake wa Kijiji cha Shilima kusherehekea kukamilika kwa mradi huo ambao ulipaswa kukamilika tangu mwaka 2013 lakini kutokana na udhaifu wa Mkandarasi haukuweza kukamilika kwa wakati.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni ya vitendo, ikiahidi inatimiza kwani ameshuhudia miradi mingi ikitekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati na kuongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo ni kama ndoto ambayo wananchi wake wamekuwa hawana uhakika wa lini itatokea hasa ikizingatiwa kwamba kero ya maji kwa wananchi hao ilikuwa ni kubwa.
Akizungumzia historia ya mradi huo, Mhe. Mansoor alisema ulianza kutekelezwa mwaka 2013 lakini Mkandarasi alikua akisuasua na baada ya Waziri kufika kwenye eneo hilo alifanikisha kuvunja mkataba na kazi ya ujenzi wa mradi huo kukabidhiwa rasmi kwa MWAUWASA. “Namshukuru sana Profesa Mbarawa, alifika hapa na kujionea hali halisi na hatimaye alifanikiwa kusitisha mkataba na Mkandarasi na kukabidhi rasmi ujenzi wa mradi kwa MWAUWASA,” alisema.
Mhe. Mansoor alitoa shukrani zake kwa Serikali kwa niaba ya wananchi wa Shilima ambapo alielezea adha waliyokuwa wakiipata kabla ya kukamilika kwa mradi huo, alisema shughuli nyingi za kimaendeleo zilisuasua kutokana na kukosekana huduma ya maji ya uhakika kwani wananchi walitumia muda mwingi kufuata maji umbali mrefu na hivyo kushindwa kushiriki kikamilifu shughuli nyingine za maendeleo.
“Kwa niaba ya wananchi wa Shilima naishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano, Waziri Mkuu alifika hapa na baadaye Waziri wa maji, waliahidi na wametimiza,” alisema Mhe. Mansoor.
Kwa upande mwingine Mhe. Mansoor aliipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA) chini ya aliyekuwa Mkurugenzi wake, Mhandisi Anthony Sanga ambaye sasa ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji kwa kukamilisha mradi huo kwa wakati kama ilivyokuwa imeagizwa na Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa. “Kwakweli MWAUWASA inafanya kazi kubwa na nzuri sana, kwa kipekee nampongeza sana Mhandisi Sanga kwa kuusimamia mradi huu kwa weledi mkubwa na sasa umekamilika,” alisema.
Naye Diwani wa Kata ya Kikubiji, Alfred Luteja aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Maji ambayo ilielekeza mradi huo ukamilishwe na MWAUWASA. “Serikali yetu ni sikivu, tumeieleza na imesikia na imefanyia kazi kilio chetu, hatimaye sasa tunatumia maji kutoka Ziwa Victoria,” alisema Luteja.
Mradi wa Shilima ulizinduliwa rasmi na Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa Septemba 14, 2019 ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Maji pamoja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inayoelekeza kuwapatia huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 85 wakazi wote waishio vijijini ifikapo mwaka 2020.