Home Mchanganyiko WATANZANIA WATAWEZESHWA ILI WASHIRIKI KUJENGA UCHUMI-MAJALIWA

WATANZANIA WATAWEZESHWA ILI WASHIRIKI KUJENGA UCHUMI-MAJALIWA

0

****************************

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania imeendelea kuchukua hatua za makusudi kwa ajili ya kuwawezesha Watanzania washiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa nchi yao, ikiwa ni pamoja na kubadilisha sera na sheria zinazohusisha sekta mbalimbali ikiwemo mafuta, madini, bima na ununuzi wa umma.

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha kuwa Watanzania wanapewa kipaumbele kwenye ajira, ununuzi wa bidhaa na huduma zao, uongezaji wa ujuzi na uhaulishaji wa teknolojia kupitia miradi hiyo ya kimkakati inayotekelezwa nchini. 

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Septemba 20, 2019) wakati wa akifungaKongamano la Taifa la Ushiriki wa Watanzania katika Miradi ya Kimkakati ya Uwekezaji (Local Content) lililofanyika kwenyeukumbi wa LAPF jijini Dodoma.

“Nyote mtakubaliana nami kuwa ushiriki wa wananchi katika uchumi wa Taifa lao ni suala linalopewa kipaumbele katika nchi nyingi duniani kwa kuwa linachangia katika kukuza uchumi wa nchi husika.” 

Amesema Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwenye huduma mbalimbali ikiwemo bima, huduma za benki, sheria na uhandisi. “Vilevile, mikataba mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu pia imetoa kipaumbele kwenye ajira za Watanzania pamoja na bidhaa na huduma ambazo zinapatikana hapa nchini.”

Waziri Mkuu amesema Serikaliya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imeweka dhamira ya dhati ya kutekeleza Sera ya Viwanda inayolenga kuipeleka nchi katika uchumi wa kati ifikapo 2025. 

Amesema jitihada za makusudi zimeendelea kufanyika ikiwa ni pamoja na kusimamia na kufanikisha utekelezaji wa malengo mbalimbali pamoja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2015/2020.

Pia, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano 2016/2017/2020/2021 ambao pamoja na mambo mengine una lenga kuimarisha upatikanaji wa stadi zinazohitajika viwandani, na stadi kwa ajili ya shughuli nyingine za uzalishaji na utoaji huduma.Amesema dhana ya ushiriki wa wananchi (Local Content) ni mojawapo ya nyenzo muhimu itakayowezesha Tanzania kufikia lengo la kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. 

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema iwapo bidhaa na huduma za Kitanzania zitatumika kwenye miradi ya kimkakati na uwekezaji unaofanyika hapa nchini viwanda vya ndani vitakua, malighafi zinazopatikana nchini zitapata soko la uhakika, ajira zitaongezeka na hivyo uchumi wa nchi utakua kwa kasi.   

“Hakuna nchi yoyote ile duniani inayoweza kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo na kufanikiwa bila ya kuweka dhamira na jitihada za makusudi za kuhakikisha kunakuwa na mazingira wezeshi kwa wananchi wake kushiriki ipasavyo kwenye shughuli za kiuchumi.”

Amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mazingira ya kisera na kisheria yanaboreshwa kwa kuzingatia maslahi ya wananchi wake, hivyo Serikali itafanya kazi kwa karibu na sekta binafsi ili kuhakikisha malengo hayo yanafanikiwa kwa kuwa sekta binafsi ina mchango mkubwa katika kujenga uchumi wa nchi na kutoa ajira kwa Watanzania.

Waziri Mkuu amesema tarehe 21 Julai 2016, wakati alipozindua Kongamo la Taifa la Ushiriki wa Watanzania katika miradi ya kimkakati aliagiza kutengenezwa kwa Mwongozo wa Taifa wa Ushiriki wa Watanzania katika Uwekezaji (National Multi-sector Local Content Guidelienes). Mwongozo huo umekamila na ameuzindua leo pamoja na  tovuti ya Miradi ya Kimkakati na Uwekezaji.

Tovuti hiyo, itakuwa na taarifa mbalimbali kuhusu miradi ya kimkakati, fursa zilizopo kwenye miradi hiyo pamoja na mipango na mikakati mbalimbali kuhusu masuala ya ushiriki wa wananchi kwenye miradi hiyo. Pia itawezesha kujenga uelewa wa umma kuhusu ushiriki wa wananchi kwenye miradi ya kimkakati na kufahamu changamoto zinazowakabili Watanzania katika ushiriki kwenye miradi mbalimbali ili kuzipatia suluhisho changamoto hizo. 

Hivyo, Waziri Mkuu ameagiza Mwongozo wa Taifa wa Kisekta wa ushiriki wa Watanzania usambazwe kwa wadau mbalimbali ili waweze kufahamu majukumu walionayo katika kuwawezesha Watanzania kushiriki katika uchumi wa nchi. “Tujenge utamaduni wa kufuatilia tovuti ya Serikali ya miradi mikubwa ya kimkakati na uwekezaji ili kutambua fursa za kibiashara.

 

Kongamano hilo limehudhuriwa na Waziri Nchi Ofisi ya Waziri Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilnith Mahenge, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi KiuchumiBeng’i Issa.

Wengine ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Salum Shamte, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi KiuchumiDkt. Festus Limbu pamoja na viongozi mbalimbali wa sekta ya umma na binafsi, wafanyabiashara, wanatlaaluma, watafiti, asasi za kiraia na vikundi mbalimbali vya wajasiriliamali.