Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Juma Aweso,akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma, wakati akiainisha mipango ya serikali katika kuwafikishia wananchi huduma ya maji ifikapo 2020, katika kikao chake na wawakilishi wa Serikali ya nchi ya Poland.
…………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
SERIKALI nchini, inatarajia kutumia kiasi cha dola milioni mia tano, ili kukamilisha ujenzi wa miradi ya maji ifikapo mwaka 2020.
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Juma Aweso, ameyasema hayo hii leo jijini Dodoma, wakati akiainisha mipango ya serikali katika kuwafikishia wananchi huduma ya maji ifikapo 2020, katika kikao chake na wawakilishi wa Serikali ya nchi ya Poland.
“Katika hili tutashirikiana na wadau mbalimbali, na ndio maana leo hii unaona tupo hapa na wawakilishi wa Serikali ya Poland kuhakikisha tunafanikisha malengo kusudiwa.” Amesisitiza Aweso.
Amesema kiasi hicho cha fedha kimelenga kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo, ambapo pia wamejadili mapendekezo mbalimbali ya miradi ya maji.
Naibu Waziri huyo amesema utatuzi wa changamoto ya maji, unatokana na azma na jitihada za Rais John Pombe Magufuli ni kumtua mama ndoo kichwani, ikiwemo kuondoa kero hiyo Vijijini na Mijini.
“Changamoto hii ya uhaba au ukosefu wa maji imekuwa ikiyakabili maeneo mbalimbali, na hivyo ni lazima kuweka juhudi kulimaliza tatizo hili kwa maeneo yote yenye uhitaji nchini.” Amebainisha Naibu Waziri Aweso.
Awali akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji (DUWASA) Mkoani Dodoma Injinia David Palanjo, amesema mradi huo utawafikia walengwa kwa wakati kama ilivyopangwa na Serikali.