Home Mchanganyiko SIMBACHAWENE AAGIZA WANAOHARIBU VYANZO VYA MAJI WACHUKULIWE HATUA

SIMBACHAWENE AAGIZA WANAOHARIBU VYANZO VYA MAJI WACHUKULIWE HATUA

0

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe.
George Simbachawene akizungumza na wananchi wa Jimbo la Kibakwe
alipofanya ziara ya kikazi wilayani Mpwapwa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe.
George Simbachawene akifurahia wimbo wa kwaya iliyoandaliwa ktumbuiza
mkutano wa hadhara aliyofanya akiwa ziarani.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe.
George Simbachawene akihutubia wananchi jimboni Kibwakwe wilayani
Mpwapwa.

Wananchi wakimkabidhi zawadi ya mbuzi Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. George Simbachawene mara baada ya
kufanya mkutano wa hadhara jimboni Kibakwe wilayani Mpwapwa.

*******************************

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe.
George Simbachawene ameagiza wanaoharibu vyanzo vya maji katika maeneo
yenye miinuko waondolewe mara moja na kuchukuliwa hatua kali za sheria.

Mhe. Simbachawene ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi wa
Vijiji vya Chogola na Makosea wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani Mpwapwa
katika Jimbo la Kibakwe ambapo alikemea tabia ya baadhi ya watu kukata miti
kwenye maeneo yenye miinuko hali inayosababisha uharibu wa vyanzo vya maji.

Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo hilo aliagiza watendaji wa kata na
vijiji kuweka alama za mipaka kwa ajili ya kulinda vyanzo vya maji yenye umbali
wa urefu wa mita 500 kila upande ili kuhakikisha wananchi hawavivamii.

"Tunapokata miti ya asili tunafanya maisha yetu kuwa magumu na vyanzo vya maji vinategemea uhifadhi wa misitu ya asili, inashangaza watu wanafyeka miti hadi kwenye milima kitakachotokea mvua ikinyesha kwa kasi ule udondo
unaporomoka na kusababisha mmomonyoko wa udongo mtakuta kijiji chote
kinasombwa," alitahadharisha.

Pamoja na hayo Simbachawene alibainisha kuwa changamoto ya mabadiliko ya
tabianchi imesababisha mabadiliko ya misimu na hivyo kuleta athari kwa
wanadamu kushindwa kuendesha shughuli za kilimo.

Aliongeza kuwa hali hii imechangia kubadilisha misimu na ndio maana wananchi
wanalalamuka kukosa mvua za kutosha kuweza kufanya shughuli za kilimo.

Akiendelea kutoa elimu kwa wananchi Waziri Simbachawene alisema kitendo
cha kukata miti kinaharibu ikolojia ya wanyama na mimea hali inayosababisha
kukosekana kwa mvua na hivyo mabadiliko ya tabianchi.

“Tarehe 23 ya mwezi huu (Septemba), Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa
marais wote kujadili namna nchi hizi zimezalisha hewa ya ukaa ambayo tunaita
kaboni kutokana na shughuli zetu wenyewe.

“Hewa ya ukaa imeongezeka na kutengeneza joto gesi ambalo linatoboa anga la
dunia ambayo ni (ozoni layer) hali husababisha misimu kubadilika na hivyo ndo
maana tunakabiliwa na changamoto ya mabadliko ya tabia nchi”. Alisema waziri huyo.