************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi watumishi wanane wa halmashauri ya wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro na kuagiza wafikishwe mahakamani kujibu tuhuma za ubadhilifu wa zaidi ya sh. bilioni tatu za mapato ya ndani.
Amesema watumishi wa umma wanawajibu wa kufanya kazi kwa bidii, maarifa na ubunifu. “Nawasihi nyote muache kufanya kazi kwa mazoea, mbadilike na kuenenda sawa na matakwa na maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Tano na anayejiona hatoshi ajiondoe.”
Waziri Mkuu amewasimamisha kazi watumishi hao leo (Jumatatu, Septemba 16, 2019) wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Ulanga kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo uliopo mjini Mahenge.
Watumishi hao kuwa ni pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Yusuph Semguruka ambaye kwa sasa amehamishiwa TAMISEMI, Rajabu Siriwa (mwekahazina), Stanley Nyange, Jonson Mwenyembole, Isack Mwansokope, Said Majaliwa, Charles Steven na Hezron Lopa.
Pia, Waziri Mkuu ametumia kikao hicho kumrejesha kazini na kumpandisha kuwa mkuu wa Idara ya Ukaguzi wa Ndani, Agustine Mwaria ambaye awali alikuwa akikaimu nafasi na kuibua ubadhilifu huo. Baada ya kuibua ubadhilifu huyo mtumishi huyo alisimamishwa kazi.
Waziri Mkuu amewataka watumishi hao wazingatie sheria, kanuni na taratibu za kiutumishi pamoja na kujiepusha na vitendo vya wizi kwa sababu wanaoathirika baada ya wao kuchukuliwa hatua za kisheria ni wenza wao na watoto.
Awali,Mkuu wa wilaya ya Ulanga, Ngollo Malenya alisema wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto wa ubadhilifu wa fedha za umma hali inayosababisha kuwepo kwa mpasuko kati ya watumishi na Baraza na Madiwani. Alisema watumishi wanaotekeleza majukumu yao ipasavyo wanaandamwa.