Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya (katikati) akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani kwenye mkutano wake na vyombo vya habari uliofanyika leo tarehe 16 Septemba, 2019. Kulia ni Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula na kushoto ni Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini, Dkt. Venance Mwase.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kulia) akifafanua jambo katika mkutano huo
………………………..
Na Greyson Mwase, Dodoma
Tume ya Madini imeitaka kampuni ya kuzalisha makaa ya mawe nchini ya TANCOAL kulipa deni la Dola za Marekani 10,408,798 ambalo ni kwa kipindi cha Septemba, 2011 hadi Juni, 2019 na kuacha kupotosha umma wa watanzania.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 16 Septemba, 2019 jijini Dodoma na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya kwenye mkutano wake na waandishi wa habari kufuatia taarifa za upotoshaji ambazo zimekuwa zikichapishwa na kampuni ya TANCOAL kupitia tovuti ya www.miningreview.com tarehe 03 Septemba, 2019 na kusambazwa kwenye mitandao mingine ya kijamii.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini, Dkt. Venance Mwase, Mkurugenzi wa Huduma za Tume, William Mtinya, Meneja wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Gift Kilimwomeshi, Meneja wa Leseni, Mhandisi Ramadhani Lwamo na Kaimu Meneja wa Utafiti na Sera, Andendekisye Mbije.
Profesa Manya alifafanua kuwa, kampuni ya TANCOAL kupitia taarifa yake ilidai kuwa, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imeanza kuitoza TANCOAL tozo ya mrabaha kwenye gharama za usafirishaji wa makaa ya mawe kutoka mgodini hadi kwa mtumiaji wa mwisho wa ndani na nje ya nchi.
Aliongeza kuwa, kampuni ya TANCOAL ilidai kulazimishwa kuuza makaa ya mawe kwa wateja wenye leseni za biashara ya madini hali itakayoongeza gharama za makaa ya mawe.
Profesa Manya alisema kuwa TANCOAL imekuwa ikilipa tozo ya mrabaha kwa kuzingatia thamani ya madini yakiwa yadi ya Kitai bila kujumuisha gharama za usafirishaji kwenda kwa wateja jambo ni kinyume na Sheria ya Madini ya Mwaka 2010.
“Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kifungu cha 87 (6) kinaelekeza namna ya kukokotoa mrabaha kwa kuzingatia thamani ya madini sokoni (kwa mtumiaji wa mwisho) ambayo inajumuisha gharama za usafirishaji hadi kwa mteja (Gross Value). Utaratibu huu wa malipo umekuwa ukifuatwa na kampuni nyingine zote zinazochimba ama kuuza makaa ya mawe isipokuwa TANCOAL,” alisema Profesa Manya.
Aliongeza kuwa, pamoja na kuelimishwa mara kwa mara juu ya namna ya kukokotoa malipo ya mrabaha kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, TANCOAL imekuwa ikikaidi kulipa mrabaha kwa kuzingatia msingi huo.
Alisema kuwa, utaratibu ambao kampuni ya TANCOAL inautumia kwa kuwauzia wateja wa makaa ya mawe katika yadi ya Kitai badala ya kusafirisha wenyewe au kutumia wafanyabiashara wa madini walioidhinishwa (Mineral Brokers or Dealers) unakwenda kinyume cha Sheria. Kifungu cha 18 (1) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kinakataza mtu au kampuni yeyote isipokuwa mmiliki halali wa leseni ya madini au mfanyakazi wa wamiliki wa leseni hizo: kumiliki, kusafirisha au kuuza madini bila kuwa na kibali cha kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria.
Alifafanua kuwa, kutokana na Kampuni ya TANCOAL kulalamikia Madai ya Mrabaha inayotakiwa kulipa Serikalini, iliundwa Timu maalum kwa ajili ya kuhakiki deni la mrabaha unaojumuisha usafirishaji wa makaa ya mawe kwa kwa kipindi cha Septemba, 2011 hadi Juni, 2014 ambayo yalikuwa hayajalipwa pamoja na kufanya upembuzi wa madai ya mrabaha ambao TANCOAL inatakiwa kulipa Serikalini kwa kipindi cha Septemba 2011 hadi Juni, 2019.
Alisema kuwa katika upembuzi na uchambuzi wa takwimu za mauzo na usafirishaji wa makaa ya mawe uliofanyika, imebainika kuwa TANCOAL inatakiwa kulipa USD 1,103,594 ikijumuisha na adhabu ya asilimia 50 kwa kipindi cha Septemba 2011 hadi Juni 2014. TANCOAL inapaswa kulipa USD 9,305,205 ikijumuisha na adhabu ya asilimia 50 kwa kipindi cha Julai 2014 hadi Juni 2019. Jumla ya malipo ni USD 10,408,798 kwa kipindi cha Septemba, 2011 hadi Juni, 2019.
Naye Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula akizungumza katika mkutano huo aliitaka kampuni ya TANCOAL kutopandisha bei ya makaa ya mawe kwa wateja na badala yake kuuza kulingana na bei elekezi zinazotolewa na Tume ya Madini kila mwezi.