…………………..
NA VICTOR MASANGU, PWANI
WAWEKEZAJI wa sekta ya viwanda wametakiwa kuhakikisha wanazingatia sheria na taratibu zote za kazi na kuachana na vitendo vya kuvunja sheria za nchi kwa kuamua kuwanyanyasa wafanyakazi wao kwa kuwanyima haki zao za msingi ikiwemo kuwapatia huduma ya matibabu,pamoja na kuwapatia maslahi yao kama inavyotakiwa bila ya kuwa na vitisho vyovyote ili kutumiza azma ya serikali ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja kwa ajili ya uwekeji wa jiwe la msingi katika kiwanda cha kutengenezea vifungashio (WANDE PRINTING) vitumikavyo katika sekta ya chakula,kilimo,viwanda, afya, ujenzi pamoja na viwanda ambacho kinajengwa katika eneo la kata ya Pangani Wilayani Kibaha na kuwaasa watendaji na mamlaka zinazohusika kuwapa ushirikiano wa kutosha wawekezaji hao bila ya ubaguzi na ubinafsi wowote.
Ndikilo alisema kwamba serikali ya awamu ya tano lengo lake kubwa ni kuendelea kushirikiana bega kwa wawekezaji mbali mbali wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Rais Dk Jojn Pombe ,Magufuli hivyo wafanyakazi wanatakiwa kupewa haki zao stahiki bila ya kuonewa hasa katika suala la vitendea kazi pindi wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
“Katika Mkoa wa Pwani kwanza nashukuru kwa sasa tunaendelea kushirikiana na wawekezaji wazawa ambao wamekuwa na nia ya kuendelea kuwekeza katika sekta ya viwanda katika maeneo mbali mbali. Lakini kila siku Rai yangu kubwa ni kuwapa haki zao zote waafanyakazi kwani wao ndio wapo mstari wa mbele katika kuzalisha bidhaa, kwa hivyo katika hili naomba sana kwa wawekezaji kuliangalia kwa jicho la tatu.”alisema Ndikilo.
Aidha Mkuu huyo aliipongeza Benki ya Azania kwa kuweza kuonyesha uzalendo kwa kushirikiana bega kwa bega na serikali ya awamu ya tano katika kuwapa sapoti na kuwawezesha mikopo wawekezaji ikiwemo kiwanda hicho kwa lengo la kuweza kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo kwa wananchi kupitia sekta ya viwanda.
Kwa upande wake mmoja wa wawekezaji wazawa katika kiwanda hicho John Obach akisoma risala kwa mgeni rasmi kwa niaba viongozi wenzake amebainisha kuwa ujenzi wa mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 6.6 na kwamba wanatarajia kutoa ajira zaidi ya 300 ambazo zitaweza kuwasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi na kuondokana na wimbi la umasikini.
Naye Mkurugenzi wa Azania Benki Charles Itembe ambao ndio wamewezesha kwa kiasi kikubwa ujenzi wa mradi huo wa kiwanda amesema kwamba lengo lao kubwa ni kuunga mkono sera ya Rais wa awamu ya tano Dr. John Pombe Magufuli ya kuwa na uchumi wa viwanda na kuahidi kuendelea kushirikiana na wawekezaji wengine katika kuinua sekta ya viwanda.
“Sisi kama taasisi ya kifedha Azania Benki nia na madhubmuni yetu makubwa ni kuhakikisha tunaaunga sera ya Rais wetu wa awamu ya tano Dk , John Pombe Magufuli katika kuwa na Tanzania ya viwanda, kwa hivyo ndio maana tumeamua kuwawezesha wenzetu wa kiwanda hiki cha kutengenezea vifungashio ili kuleta mapinduzi ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Pia liongeza kwa sasa wataendelea kutoa sapoti kwa wadau wa maendeleo pamoja na serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata fursa mbali mbali za ajira kupitia miradi ya ujenzi ywa viwanda ambavyo vinajengwa katika maeneo tofauti lengo ikiwa ni kuondokana na wimbi la umasikini na jukikwamua kiuchumi.