Sehemu ya watumishi wa wizara ya kilimo wakifuatilia maelekezo ya kazi waktika wa kikao na Waziri wa Kilimo jana Jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba akizungumza wakati wa kikao kazi na watumishi wa wizara hiyo jana Jijini Dodoma ambapo amewataka kutumia vizuri fedha za umma.
Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe akizungumza wakati wa kikao kazi na watumishi wa wizara hiyo jana ,Jijini Dodoma.
************************
Dodoma, 14 Septemba, 2019
Waziri wa Kilimo Japeth Hasunga amewaagiza watumishi wa wizara yake
kufanya kazi kwa uadilifu na uzalendo ili kuongeza uzalishaji wa mazao
nchini.
Amewataka wataalamu kuzingatia dira ya wizara ili kukifanya kilimo kuwa
cha kibiashara na cha faida kwa wakulima kote nchini.
Waziri Hasunga ametoa agizo hilo Ijumaa (13.09.2019) wakati alipofanya
kikao cha kazi na wafanyakazi wote wa wizara ya kilimo waliopo makao
makuu Jijini Dodoma.
“Lengo la wizara yetu ni kuhakikisha nchi inazalisha mazao ya kutosha na
kuwa na utoshelevu na usalama wa chakula muda wote” alisema Waziri.
Alieleza katika kikao hicho kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula
umewezesha nchi kuwa na utoshelevu asilimia 124 mwaka 2018 na
asilimia 119 mwaka 2019.
Waziri Hasunga aliwataka watumishi wa wizara hiyo kuweka mipango
inayotekelezeka kitaalam ili kujibu hitaji la wakulima nchini ikiwa ni pamoja
na elimu ya kilimo cha kisasa na chenye tija katika eneo dogo.
“Andikeni miradi ili wizara ipate pesa zaidi za kutekeleza shughuli za
uzalishaji mazao nchini na badala ya kutegemea bajeti ya serikali ili kufikia
tija ya uzalishaji” Waziri Hasunga.
Alisema Tanzania ina hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo cha mazao
mbalimbali lakini hali ya uzalishaji imeendelea kushuka kila mwaka
kutokana na wataalam kutotimiza majukumu yao.
Ili kufikia uzalishaji mkubwa na wenye tija amewashauri wataalam wa
wizara ya kilimo kujifunza uzoefu na teknolojia iliofikiwa na nchi za
Kenya,Rwanda na Israel ambazo zimepiga hatua kubwa kuzalisha mazao
katika eneo dogo.
“Israel, Rwanda na Kenya wanafanya vizuri katika uzalishaji,kajifunzeni ili
tubadilishe kilimo chetu kiwe na mchango mkubwa zaidi kwenye pato la
taifa ” alisisitiza Waziri.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba akizungumza
kwenye kikao hicho aliwasihi wafanyakazi kujituma na kutumia vizuri fedha
za umma ili miradi inayotekelezwa na wizara iwanufaishe wakulima.
Mgumba aliwataka watumishi hao kuongeza weledi wa ufanyaji kazi ili
kupunguza gharama za uzalishaji na mkulima apate bei nzuri ya mazao
yake sokoni.
Naye Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe alisisitiza suala la matumizi ya
Tehama kuzingatiwa katika kuongeza ufanisi wa kazi za wizara ikiwa ni
pamoja na upatikanaji wa takwimu sahihi za mazao na utendaji kazi.
Bashe aliwakumbusha watumishi hao kuwa wizara ya kilimo ndio imeajili
watu asilimia 70 hivyo mafanikio ya utekelezaji wa Ilani yakiendelezwa
yatasaidia Chama cha Mapinduzi kuendelea kuungwa mkono na wananchi.
“Uwepo wa Chama cha Mapinduzi madarakani utaimarika zaidi endapo
sekta hii ya kilimo iliyoajili watanzania wengi itatoa mchango unaokusudiwa
katika uchumi”alisema Naibu Waziri Bashe.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Matherw Mtigumwe
alimshukuru na kumhakikishia Waziri Hasunga kuwa wataalam walio chini
yake wataongeza kasi katika ufanyaji kazi ili wizara ifikie malengo ya nchi .
Wizara ya kilimo ina watumishi 974 kati yao watumishi 452 wapo makao
makuu na wengine 522 wapo kwenye taasisi, vyuo na wakala nchini.