Home Mchanganyiko HALMASHAURI YA WILAYA YA KIBAHA YAJIPANGA KUDHIBITI MIANYA YA WAKWEPA USHURU

HALMASHAURI YA WILAYA YA KIBAHA YAJIPANGA KUDHIBITI MIANYA YA WAKWEPA USHURU

0

MWAMVUA MWINYI,KIBAHA

BAADHI ya madiwani katika halmashauri ya wilaya ya Kibaha,Pwani wameielekeza halmashauri hiyo kuangalia namna ya kuongeza mashine( posi )na mageti kwenye maeneo ambayo yanaonekana ni njia za panya zinazotumika kukwepa ushuru.

Hatua hiyo wameieleza ,inalenga kuinua mapato ya ndani ,kudhibiti utoroshaji na kudhibiti mianya ya wizi.

Wakizungumzia kwa nyakati tofauti, wakati wa baraza la madiwani, diwani wa kata ya Dutumi Mkali Kanusu na diwani wa Kilangalanga Mwajuma Denge walisema, yapo maeneo ambayo makusanyo yanashuka kutokana na kukosa posi na mengine watu kukwepa kulipa ushuru.

Denge alisema, kumekuwa na wimbi kubwa la kutorosha mkaa pasipo kulipia ushuru eneo la Ruvu Madimla kutokana na kutokuwepo geti.

Aliomba kwa mkurugenzi, kuweka geti pamoja na Mzenga Njiapanda ili kudhibiti upotevu wa mapato.

Nae Kanusu alifafanua, suala la mapato ni la wote ambapo inastahili kusimamia wakusanyaji wa ushuru kwenye vizuizi na kuangalia namna ya kuongeza nguvu pasipo kuwepo mageti.

“Pia watendaji wa kata watoe taarifa ya makusanyo kwa madiwani,kutuambia kilichopatikana na changamoto zinazokwamisha kuongeza makusanyo,tubadilishe utaratibu wa kufanya tathmini wenyewe kuanzia kata,hii itatusaidia”alielezea Kanusu.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo,Butamo Ndalahwa alieleza, wanakusudia kuinua mapato katika vyanzo vya mapato ya ndani kwa kufanya ukaguzi wa kushtukiza na kusimamia kikamilifu vizuia vyote .
Alielezea kuwa mbali ya hilo ,wameanza kudhibiti baadhi ya mageti ikiwemo geti la Madege kutoka makusanyo 0 hadi sasa wanakusanya milioni mbili kwa wiki.
“Kamati ya fedha tunatenga muda na kutembelea miradi mbalimbali na mageti hayo ambapo maeneo yasiyoridhisha wameongeza usimamizi na kuongeza mageti katika sehemu zinazotumiwa kukwepa kodi”alieleza
Alibainisha ,ili kuongeza msukumo wanatarajia kuanza kushindanisha kata kwa kata na kutoa zawadi kwa kata itakayoongoza kwa makusanyo.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Mansoor Kisebengo alisema makisio ya makusanyo ya ndani yalikuwa bilioni 2.164.210, hali halisi ya makusanyo hadi sasa ni bilioni 1.370.278 sawa na asilimia 63.
Kisebengo aliainisha,wamepokea asilimia 80 ya mapato kutoka serikali kuu,hivyo aliiasa halmashauri na madiwani kujipanga kupitia mapato ya ndani ili kusonga mbele na kuleta maendeleo kwa wananchi wa Kibaha.