Home Mchanganyiko SERIKALI YAJIPANGA KUTATUA TATIZO LA MAJI SIMANJIRO

SERIKALI YAJIPANGA KUTATUA TATIZO LA MAJI SIMANJIRO

0

 

Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) akisomewa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa maji wa Olchoronyori na Mhandisi wa Maji wa Wilaya Eng. Joanes Mathew.

Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) akitoka kukagua mradi wa maji wa Olchoronyoi.

Waziri wa Maji Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Simanjoro Eng. Zephania Chaula na wananchi wa kijiji cha Olchoronyoi mara baada ya kumaliza kukagua mradi wa maji wa Olchoronyoi na kuzungumza nao.

Waziri wa Maji Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) akipata maelezo kutoka kwa mmoja wa wasimamizi wa Kampuni ya Jandu Plumbers Ltd. inayotekeleza mradi mkubwa wa maji wa Orkesumet.

……………..

Serikali imejipanga kuhakikisha inamaliza tatizo la maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Simanjro mkoani Manyara. 

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) alipokuwa akizungumza na wananchi wa Simanjiro mara baada ya kukagua miradi ya maji ya Naisinyai, na mradi mkubwa wa Orkesumet.

Waziri Mbarawa alisema ili kukamilisha mradi wa maji wa Naisinyai serikali itatoa kiasi cha fedha Tsh. milioni 80 mwezi huu Septemba, 2019 kwa kazi ya kulaza mabomba ili wananchi wa Mirelani waweze kupata majisafi na salama. 

Alisema, kazi ya kulaza mabomba itafanywa na wataalam wetu wa ndani na kusimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Babati (BAWASA). 

Aidha, Prof. Mbarawa alitembelea mradi mkubwa wa maji wa mji wa Orkesumet  unaotekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na BADEA na OFID kupitia mkopo wa masharti nafuu ambao umetengewa jumla ya Dola za Marekani Milioni 18.42. 

BADEA ni (Benki ya Maendeleo ya Nchi za Kiarabu kwa nchi za Afrika) na OFID ni (Mfuko wa Maendeleo wa nchi zinazozalisha mafuta) ambao wanatoa Dola za Marekani Milioni 8 kila moja na Serikali ya Tanzania inachangia kiasi cha Dola za Marekani Milioni 2.42.

Mradi huu utakapo kamilika utakuwa na uwezo wa kuhudumia wakazi 52,000 na mifugo katika mji wa Orkesumet pamoja na vijiji vinavyozunguka mji huo. 

Hata hivyo, Waziri Mbarawa hakuridhishwa na kasi ya utekelezaji ya ujenzi wa chanzo  (intake) na mtambo wa kutibu maji (treatment plant) inayofanywa na mkandarasi anayetekeleza mradi huu mkubwa wa Orkesumet Jandu Plumbers Ltd ya Tanzania.

“Ongezeni kasi ya utekelezaji ili mradi huu ukamilike kwa haraka na wananchi waweze kupata majisafi na salama na ikiwezekana fanyeni kazi usiku na mchana”, alisema Prof. Makame Mbarawa.

Naye Mkuu wa Wilaya Simanjiro Eng. Zephania Chaula amemshukuru sana Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa kwa kufanya ziara ya kukagua miradi ya maji Wilayani Simanjiro. 

Alisema, ziara hiyo imewapa matumani makubwa wananchi wa Simanjiro ambao wanachangamoto kubwa ya upatikanaji wa majisafi na salama.