Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim M. Majaliwa akiagana na Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) Bw Filippo Grandi mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo baina yao kuhusu wakimbizi waliopo Tanzania. Mazungumzo hayo yamefanyika Yokohama, Japan.
……………………
SERIKALI ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) katika kutatua changamoto zinazotokana na uwepo wa wakimbizi nchini pamoja na kutafuta suluhu ya kudumu kwenye nchi zao ili wakimbizi hao waweze kurejea makwao kuendelea na shughuli za maendeleo.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo (Ijumaa, Agosti 30, 2019) katika mazungumzo yake na Kamishna Mkuu wa UNHCR, Bw. Filippo Grandikwenye Kituo cha Maonyesho cha Yokohama nchini Japan baada ya kuhitimishwa kwa Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (Tokyo International Conference on African Development – TICAD 7).
Katika mazungumzo hayo, Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa UNHCR kuisaidia mikoa inayokaliwa na wakambizi kutokana na kuharibiwa kwa mazingira. “Hata hivyo Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na UNHCR kuimarisha ulinzi wa maeneo ya wakimbizi ili wananchi wa maeneo hayo waendelee kuishi kwa amani na utulivu.”
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), Bw. Filippo Grandi amesema amefurahishwa na utayari wa Serikali ya Tanzania katika kupokea wakimbizi na usikivu wa Rais Dkt. John Magufuli katika kushughulikia changamoto za wakimbizi.
Waziri Mkuu yupo nchini Japan akimwakilisha Rais Dkt. John Magufuli kwenye Mkutano wa Kilele wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (Tokyo International Conference on African Development – TICAD 7) ambao umehitimishwa leo.
Waziri Mkuu ameambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi na viongozi mbalimbali kutoka Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.