Home Mchanganyiko SIMANJIRO YAZINDUA SOKO LA MADINI

SIMANJIRO YAZINDUA SOKO LA MADINI

0
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara mhandisi Zephania Chaula akishiriki kukata utepe na wadau wa madini kwenye uzinduzi wa soko la madini ya vito Orkesumet.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara mhandisi Zephania Chaula akizungumza kwenye uzinduzi wa soko la madini ya vito Mji mdogo wa Orkesumet.
Matukio mbalimbali kwenye uzinduzi wa soko la madini ya vito Mji mdogo wa Orkesumet Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara
…………………..
MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mhandisi Zephania Chaula amezindua soko la madini ya vito kwenye mji mdogo wa Orkesumet.
Soko hilo litatumika kuuza na kununua madini ya vito ikiwemo Ruby, Green Tomarine, Green Gainet, Tanzanite na mengineyo.
Mhandisi Chaula akizungumza wakati akizindua soko hilo, amewataka wafanyabiashara na wachimbaji wa madini kutumia soko hilo kuuza madini na kulipa kodi ya serikali. 
Chaula alisema serikali imelenga kuondoa ukiritimba kwenye sekta ya madini hivyo wachimbaji na wanunuzi watumie fursa hiyo kwa kuuza na kununua madini kwenye soko hilo. 
“Baada ya kumaliza uzinduzi wa soko hilo la madini Orkesumet tutazindua soko lingine Mirerani hivyo kuwa na masoko mawili kwenye mkoa wa kimadini wa Simanjiro hiyo ni hatua kubwa mno,” alisema mhandisi Chaula. 
Aliwataka wafanyabiashara na wachimbaji kutumia masoko hayo kulipa kodi kwani ndizo zinazotumika kwenye maendeleo mbalimbali ya jamii. 
“Mnaona pale tunajenga hospitali ya wilaya ya Simanjiro, awali hatukuwa nayo ila kupitia makusanyo ya ndani yanayotokana na kodi zenu na usimamizi wa Rais John Magufuli hivi sasa tumekamilisha hospitali,” alisema mhandisi Chaula. 
Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara (Marema) Justin Nyari alimpongeza mkuu huyo wa wilaya na ofisi ya madini kwa kuhakikisha soko hilo linafanikishwa kuanzishwa ili kutimiza agizo la Rais John Magufuli. 
Nyari alisema wanamuomba mkuu huyo wa wilaya kupeleka salamu zao kwa mkuu wa Mkoa huo Alexander Mnyeti ili azifikishe kwa Rais John Magufuli kwani anawapenda na kuwapa kipaumbele wachimbaji na sekta ya madini kwa ujumla. 
Kaimu ofisa madini mkazi mkoa wa kimadini wa Simanjiro mhandisi Castro Maduwa alisema wamejipanga kuvuka lengo la makusanyo ya kodi ya sh6 bilioni kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020.
Maduwa alisema mwaka jana 2018/2019 walipangiwa wakusanye sh1.5 bilioni lakini wakakusanya sh2.8 bilioni hivyo kuvuka lengo. 
Katibu wa CCM wa wilaya ya Simanjiro Ally Kidunda alisema ilani ya uchaguzi wa CCM inazidi kutekelezwa kwa vitendo Simanjiro. 
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Sendeu Laizer alipongeza hatua hiyo kwani itaongeza tija kwa wachimbaji na wanunuzi wa madini Simanjiro.