******************
Na. Angela Msimbira OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.
Selemani Jafo ameziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanaweka
mikakati kwa kubuni miradi ambayo itawasaidia katika kujiwekea vitega
uchumi na kukuza mapato katika Halmashauri zao ili kuachana na
utegemezi katika Serikali.
Ameyasema hayo leo wakati wa utiaji wa saini Miradi ya Ujenzi wa
majengo mawili ya vitega uchumi vya Halmashauri ya Jiji la Dodoma
uliofanyika katika Viwanja vya Nyerere Square, Jijini Dodoma.
Mhe. Jafo amesema Halmashauri zote nchini zinatakiwa kuwa wabunifu,
kujipanga na kuweka mikakati ya kuondokana na unyafuzi wa mapato kwa
kuanzisha miradi ambayo itasaidia kuongeza mapato na kuleta maendeleo
kwa jamii.
Amesema kuwa kama Halmashauri zote zingekuwa wabunifu na kuamua
kujitoa katika utendaji kazi kusingekuwa na unyafuzi wa mapato bali
zingejikita katika kubuni na kuibua miradi ya maendeleo ili kujikwamua
kiuchumi na kujiongezea vitega uchumi vitakavyoleta maendeleo katika
Halmashauri zao.
“ Kusipokuwa na ubunifu, kujitoa katika utendajikazi wa watumishi wa
Halmashauri, hali ya unyafuzi wa mapato itaendelea na bado Halmashauri
nyingi zitakuwa ni tegemezi kwa Serikali, hivyo ninaziagiza Halmashauri
zote nchini kuhakikisha wanabuni vitega uchumi ili waweze kujitegemea
kwa kutumia mapato yao ya ndani ” Anasisitiza Mhe.Jafo.
Mhe. Jafo amezitaka Halmashauri zote nchini kuiga mfano wa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma kwa kubuni Miradi ya Maendeleo kwa ajili ya vitega
uchumi na kuondokana na utegemzi kwa Serikali.
Amefafanua zaidi kuwa watumishi wa Serikali za Mitaa nchini kuacha
kufanyakazi kwa maigizo, kwa kujionyesha kwenye mitandao bali
wafanyekazi kwa weledi lengo likiwa ni kuwahudumia wananchi maskini
na kulipeleka taifa katika uchumi wa kati.
“Kuna watu nchi hii wamezoea maigizo, hivyo kwa wale ambao wapo chini
ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuacha kufanyakazi
kwa maigizo bali watu wafanyekazi kwa weledi ili kufikia mallengo ya
Serikali.” Amesisitiza Mhe. Jafo.
Amesema watu wasipende kujionyesha kwenye mitandao kuwa
wanafanyakazi , bali wafanye kazi kwa ajili kulitumikia taifa hasa wananchi
maskini kwa kuwa nchi hii inabadilika na kinachohitajika ni maendeleo ya
Taifa.
Amewasii vijana waliopewa dhamana ya uongozi nchini kufanyakazi kwa
bidii na maarifa waliyonayo na kuacha kufanyakazi kwa maigizo, lengo
likiwa ni kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John
Pombe Magufuli katika kufikia uchumi wa kati.
Amewapongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuweza kutumia
Makusanyo ya Fedha za Ndani kwa ajili ya ujenzi wa vitega uchumi lengo
kubwa ni kutoa unyafunzi wa mapato na kupunguza utegemezi kwa
Serikali.
Wakati huohuo Mkurugenzi wa Halmashauri wa Jiji la Dodoma Bw.
Godwin Kunambi amesema ujenzi wa jengo la Hoteli “Dodoma City Hotel”
litajengwa katika eneo la Paradise barabara ya Nyerere kwa gharama ya
shilingi bilioni 9.9 kutoka katika nyanzo vya mapato ya ndani lengo likiwa
ni kupunguza utegemezi kwa Serikali, kuongeza ajira kwa wananchi wa
Dodoma, kutoa huduma bora kwa wananchi, kuboresha mji wa Dodoma na
kupunguza umaskini na kuongeza kipato kwa wananchi wa Dodoma.
Bw. Kunambi ameendelea kusema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma
inategemea kujenga kitega uchumi Mji wa Serikali “Government City
Complex “kwa gharama ya shilingi bilioni 59.3 ambapo kutakuwa na ofisi,
maduka,Kumbi za Mikutano, Maegesho ya Magari, Maeneo ya mabenki,
migahawa bna maeneo ya mahoteli.
Aidha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt. Bilinith Mahenge amesema
kuwa kupitia miradi hiyo Wananchi wa Mkoa wa Dodoma watapata fursa
ambazo zitawasaidia kuongeza kipato na kukuza uchumi wa Dodoma
utaongezeka.