Home Mchanganyiko WAZIRI MHAGAMA AFUNGUA WARSHA YA WADAU KUJADILI FURSA ZA BOMBA LA MAFUTA...

WAZIRI MHAGAMA AFUNGUA WARSHA YA WADAU KUJADILI FURSA ZA BOMBA LA MAFUTA –DODOMA

0
????????????????????????????????????

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, bunge, kazi, vijana, ajira na watu wenye ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama akitoa hotuba yake wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku moja ya majadiliano ya wadau kuhusu ushiriki wa Watanzania katika miradi ya kimkakati (Local content) katika sekta ya uziduaji mkoani Dodoma iliyofanyika tarehe 26 Agosti, 2019.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, bunge, kazi, vijana, ajira na watu wenye ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama akisalimiana na mmoja wa washiriki wa warsha hiyo Bi. Mariagorete Charles mara baada ya ufunguzi wa warsha hiyo Agosti 26, 2019.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia sera, bunge, kazi, vijana, ajira na watu wenye ulemavu Mhe.Jenista Mhagama akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt. Bilinith Mahenge mara baada ya kufungua warsha ya majadiliano ya wadau kuhusu ushiriki wa Watanzania katika miradi ya kimkakati (Local content) katika sekta ya uziduaji mkoani Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt. Bilinith Mahenge pamoja na sehemu ya washiriki wa warsha hiyo wakifuatilia mada kutoka kwa mwezeshaji Bi. Mariagorete Charles kutoka katika mradi wa EACOP (hayupo pichani) wakati wa warsha hiyo.

Sehemu ya washiriki wa  warsha hiyo wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, bunge, kazi, vijana, ajira na watu wenye ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akitoa hotuba yake wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo.

Mwasilishaji wa mada kuhusu mradi ya bomba la mafuta – EACOP Bi. Mariagorete Charles akiwasilisha mada wakati wa warsha hiyo kwa washiriki wa warsha iliyofanyika Agosti 26, 2019 Jijini Dodoma.

*****************

NA.MWANDISHI WETU

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe.Jenista Mhagama amefungua warsha ya siku moja ya majadiliano ya wadau kuhusu ushiriki wa Watanzania (Local content) katika sekta ya uziduaji mkoani Dodoma.

Warsha hiyo imewakutanisha pamoja wawakilishi zaidi ya 100 wa makundi mbalimbali kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Dodoma ili kujadili mikakati na maendeleo ya utekelezaji wa dhana ya ushiriki wa Watanzania katika fursa za miradi ya kimkakati ikiwemo mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima nchini Uganda kwenda Tanga, Tanzania na sekta ya madini kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa kufungua warsha hiyo leo Agosti 26, 2019 katika ukumbi wa Kilimanjaro Hazina Mjini Dodoma Waziri Mhagama aliwataka viongozi wa maeneo ambako bomba litapita wawahamasishe wananchi kuchangamkia fursa zitakazokuwepo katika utekelezaji wa mradi huo na kujiletea maendeleo.

“Ni wakati sahihi sasa kuitumia fursa hii ya miradi mikubwa ambayo inalenga kunufaisha wananchi kwa kuzingatia kuwa ajira zitazalishwa kwa wazawa hivyo mjiandaae kikamilifu katika kuupokea mradi huu,” alieleza Mhagama.

Waziri Mhagama aliongezea kuwa, Sheria ya Mafuta imeweka wazi kwamba watanzania na kampuni za kitanzania zinatakiwa zipewe kipaumbele wakati wa ununuzi. Serikali inaamini kwamba Sekta binafsi ina mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa nchi. Hivyo ni matarajio  kwamba Mkandarasi wa mradi atazingatia matakwa ya Sheria hii na pale ambapo kampuni za kitanzania hazina uwezo basi ziingie ubia na kampuni za nje ili kuongeza ujuzi wa uzalishaji na utoaji wa huduma.

Alifafanua kuwa, kwa kuzingatia dhamira ya Serikali ya awamu ya Tano kuona Watanzania wanamiliki uchumi wao, hivyo wataendelea kuwahamasisha watanzania  kushiriki katika miradi Mikubwa ya kimkakati na katika miradi mbalimbali.

“Serikali kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchu Kiuchumi imejipanga kuweka mazingira wezeshi kwa watanzania ikiwa ni pamoja na kutengeneza Sera na Sheria na miongozo inayotoa kipaumbele kwa watanzania kupata fursa za ajira, kushiriki kwa kutoa huduma, uuzaji wa bidhaa na utoaji wa huduma kwenye miradi inayotekelezwa hapa nchini hasa katika sekta ya uziduaji,”alisisitiza Mhagama.

Mradi wa EACOP ni moja kati ya miradi mikubwa ambao una manufaa mengi kwa nchi yetu na kueleza kuwa, bomba hili la mafuta ghafi litakuwa na urefu wa km 1443 kati ya hizo km 296 zitakuwa nchini Uganda na km 1147 zitakuwa Tanzania. Hii ni fursa kubwa kwa watanzania kwa kuwa 80% ya mradi huu utapita Tanzania.

Aidha alibainisha mikoa itakayopitiwa na mradi huo ikiwemo Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga na kufafanua kuwa bomba hilo litapita katika wilaya 24, Kata 134 na vijiji zaidi ya 180 na kutoa wito kwa wananchi kujiandaa na kuhakikisha wanaandaa mazingira wezeshi katika kushiriki fursa zitakazotokana na uwepo wa mradi huo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt. Bilinith Mahenge alipongeza jitihada zinazoendelea katika kuhamasisha na kutoa elimu kwa jamii juu ya ushiriki wa Watanzaia katika fursa ya mradi bomba la mafuta na kuahidi kuzimamia kikamilifu ili kuhakikisha jamii inashiriki kwa uhakika.

“Kipekee ninapongeza juhudi zinazoendelea katika kuhakikisha wananchi wanajikwamua kiuchumi kwa kuzingatia ujio wa miradi hii ya kimkakati nchini hivyo hatuna budi kuendelea kutoa rai kwa Watanzania wote kuchangamkia fursa hizi,”alisema Dkt. Mahenge.