Home Michezo VODACOM YAREJESHA UDHAMINI LIGI KUU, YASAINI MKATABA WA MIAKA MITATU KWA SH...

VODACOM YAREJESHA UDHAMINI LIGI KUU, YASAINI MKATABA WA MIAKA MITATU KWA SH BILIONI 9

0

Na Saada Salim, DAR ES SALAAM
KAMPUNI ya Vodacom Tanzania jana imesaini mkataba wa miaka mitatu kurejesha udhamini katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya mwaka mmoja wa kujiweka kando kufuatia kutofautiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Vodacom haikusaini mkataba mpya wa kuendelea kudhamini Ligi Kuu msimu uliopita kufuatia kutofikia makubaliano na TFF, huku sababu kubwa ikielezwa ni ongezeko la timu kutoka 16 hadi 20.
Lakini baada ya makubaliano ya kupunguza idadi ya timu kuanzia msimu huu, jana Vodacom na TFF wameingia mkataba huo wenye thamani ya Shilingi Bilioni 9, yaani Sh Bilioni 3 kwa mwaka, ikiwa ni ongezeko la Sh Bilioni 2.4 kutoka mkataba uliomalizika mwaka 2018.Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba huo jana makao makuu ya Vodacom mjini Dar es Salaam, Rais wa TFF Wallace Karia amesema kwamba udhamini huo utaleta matokeo chanya na watatoa ushirikiano kwa muda wote wa mkataba.
Karia amesema Uendeshaji wa Mpira wa Miguu una gharama kubwa,wanawakaribisha Vodacom kushirikiana na wadhamini wengine.
Rais Karia ameongeza kuwa Kuongezeka kwa idadi ya timu kwenye mashindano ya CAF kufikia 4 ni kielelezo tosha cha kuimarika kwa Ligi Kuu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Vodacom Hisham Hendi amesema ni furaha kubwa kuingia mkataba wa kuidhamini Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Hendi amesema Katika mipango yao ni kuona siku moja watazamaji wanaoingia uwanjani wanapata urahisi wa kununua tiketi kupitia huduma ya Mpesa.
Naye Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dk. Harrison Mwakyembe ameipongeza TFF kwa hatua ya kusaini mkataba na Vodacom kudhamini Ligi Kuu.
Amesema Vodacom wameona uendeshaji bora wa TFF ambayo inaaminika na wanaingia katika moja ya Ligi Bora duniani.